TOKYO-Mwanariadha maarufu kutoka Tanzania, Alphonce Simbu ameibuka mshindi wa mbio ndefu (Marathon) katika mashindano ya riadha ya dunia yanayofanyika nchini Japan.
“Nimeweka historia leo, ikiwa ni medali ya kwanza ya dhahabu ya Tanzania katika mashindano ya dunia,”amesema Simbu baada ya ushindi wake.
“Nakumbuka mwaka 2017, kwenye mashindano ya dunia ya London, nilishinda medali ya shaba. Kisha nilikimbia mara nyingi lakini sikupata medali yoyote, hivyo hatimaye ni hapa, nilijiambia kuwa sitakata tamaa.”
Simbu ameshinda mbio hizo mapema leo Septemba 15, 2025, baada ya kutumia muda wa saa 02:09:48, hivyo kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu katika mbio ndefu za dunia.
Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan amempongeza Simbu kwa ushindi huo.
"Hongera sana Alphonce Simbu kwa Medali ya Dhahabu ya ushindi wa Mbio Ndefu za Mashindano ya Kimataifa ya Riadha ya Tokyo. Ndani ya saa 2:09:48 umeandika sehemu ya historia ya Taifa letu.
"Kama nilivyokusihi uliposhika nafasi ya pili kwenye Boston Marathon mwezi Aprili mwaka huu, ushindi wako ni matokeo ya nidhamu yako ya hali ya juu na kujituma kwa bidii kwenye kazi.
"Umekuwa mfano bora kuhusu nguzo hizo mbili za kazi kwa wanariadha na wanamichezo wenzako, na hata kwa wasiyo wanamichezo. Endelea kuipeperusha vyema na kuiheshimisha bendera ya Taifa letu,"amefafanua Rais Dkt.Samia.
Tags
Alphonce Simbu
Breaking News
Habari
International Marathon
Japan Marathon
Mbio za Kimataifa
Michezo

