MOROGORO-Mahakama ya Wilaya ya Morogoro imemtia hatiani askari mhifadhi wa Hifadhi ya Asili ya Mlima Uluguru, Bernard Mwaituka kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2023.
Katika shauri la rushwa namba 23268/2025, Mahakama ilielezwa kuwa, mshtakiwa alipokea kiasi cha shilingi 450,000 kwa ahadi ya kuachilia mbao pamoja na mashine za kukatia mbao (chain saw) ambazo alikuwa amezikamata kwa madai kuwa hazikuwa na vibali halali.Hakimu Mheshimiwa Victor Kitauka, baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, alimtia hatiani Mwaituka na kumhukumu kulipa faini ya shilingi 500,000 au kifungo cha miaka mitatu jela, pamoja na kurejesha shilingi 450,000 alizokuwa amepokea kwa njia ya hongo.
Mshtakiwa aliamua kulipa faini pamoja na kurejesha fedha hizo ili kuepuka kifungo cha jela.
Shauri hilo liliendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Husna Kiboko na Bi. Felister Chamba.
Hukumu hiyo ni ushahidi kuwa,vyombo vya dola havitasita kuchukua hatua kali kwa watu au watumishi wa umma wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, hasa vinavyohatarisha rasilimali za taifa kama misitu.
Tags
Askari Mhifadhi
Breaking News
Habari
Mahakamani Leo
PCCB Tanzania
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)