DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Rwanda (NBR) katika kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali ya kustawisha sekta ya fedha na uchumi wa nchi zote mbili.

Gavana Tutuba ameyasema hayo Septemba 9,2025 alipokutana na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Mhe.Jenerali Patrick Nyamvumba, ambaye alitembelea ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Jenerali Nyamvumba aliipongeza Benki Kuu kwa kuwa na ubunifu unaoleta mageuzi katika sekta ya fedha nchini hususan katika mifumo ya malipo ambayo inarahisisha ufanyaji wa biashara nchini humo pamoja na mpango wa Benki Kuu wa ununuzi wa dhahabu.
Aliongeza kuwa Benki Kuu ya Rwanda inakusudia kujifunza namna BOT inavyosimamia mifumo ya malipo ya taifa na inavyotekeleza mpango wa ununuzi wa dhahabu kwa ajili ya kutunisha akiba ya fedha za kigeni.
Kwa upande wake Gavana ,Bw. Emmanuel Tutuba alimueleza Balozi huyo kuwa Benki Kuu ya Tanzania kupitia wataalam wake wa ndani imetengeneza Mfumo wa Malipo wa Papo kwa Hapo (TIPS) ambao umeleta mageuzi makubwa kwenye urahisi na unafuu wa kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki nchini.
Aliongeza kuwa uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili unaleta chachu ya kuendelea kufanya maboresho ya mifumo ya malipo ili kurahisisha na kuongeza idadi na kiasi cha miamala inayofanyika kati ya Tanzania na Rwanda.
Kuhusu mpango wa ununuzi wa dhahabu Gavana alisema kuwa tangu tarehe 1 Oktoba 2024 Benki Kuu ilipoanza rasmi ununuzi wa dhahabu hadi kufikia Agosti 2025, jumla ya tani 9.165 za dhahabu zenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 1,015.98 zimekwishanunuliwa.


