BoT yatunukiwa Tuzo ya Kimataifa kwa ubunifu wa mifumo ya malipo ya kisasa

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetunukiwa Tuzo Kuu ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr.Financial Inclusion Innovation Award) kutokana na utekelezaji madhubuti wa mifumo ya malipo ya kisasa, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za kufanya miamala kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa huduma za kifedha nchini.

Tuzo hiyo imetolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI) inayoundwa na benki kuu na taasisi nyingine za udhibiti wa kifedha kutoka nchi 84 zinazoendelea duniani.
Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Bi. Lucy Shaidi amewaeleza waandishi wa habari leo Septemba 16,2025 katika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam kuwa, mojawapo ya mafanikio makubwa yaliyoiweka Benki Kuu katika nafasi hiyo ni Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo unaofahamika kama Tanzania Instant Payment System (TIPS).

Bi.Shaidi amesema, mfumo huo umeongeza urahisi wa kufanya miamala ya kifedha baina ya benki na watoa huduma wa kifedha wa kidijitali kwa wakati, hivyo kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini.

Aidha, mafanikio mengine yametokana na matumizi ya msimbo milia wa malipo (QR Code) unaofahamika kama TANQR, ambao umeanzishwa ili kuwezesha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kupokea malipo kwa urahisi kupitia simu au benki.

"Mchango wa Benki Kuu kwenye ubunifu huu umeonekana katika machapisho mbalimbali duniani ambayo Benki Kuu iliyafanya juu ya mfumo wa TIPS na TANQR.

"Pia Benki Kuu imekua mstari wa mbele katika kugawa ujuzi kwa nchi nyingine kwenye ubunifu huu ikiwemo nchi za Kenya, Lesotho, Rwanda na Uganda."

Pia, amesema mafanikio haya ya ubunifu umewezesha kuona ongezeko la miamala kwa mwaka wa fedha 2024/25 kufikia miamala milioni 560 yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 41.

Vilevile katika kipindi hicho, miamala ya kutumia msimbomilia na LipaNamba iliweza kufika milioni 60 na thamani ya takribani shilingi trilioni 4.

Kupitia maboresho haya ya teknolojia ya malipo, Benki Kuu imeendelea kuonesha dhamira ya kukuza uchumi wa kidijitali na kuhakikisha kuwa wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma rasmi za kifedha.

"Tuzo hii mashuhuri inalenga kutambua nchi wanachama wa AFI ambao wameonesha juhudi kubwa katika ubunifu na matumizi ya teknolojia, pamoja na kutambua uongozi imara katika kuchochea kasi ya upatikanaji na matumizi ya Huduma Jumuishi za Fedha.

"Tanzania ni mwanachama wa taasisi hiyo kupitia Benki Kuu kuanzia mwaka 2011."

Bi.Shaidi amesema, tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Gavana anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Huduma Jumuishi za Fedha uliofanyika mjini Swakopmund, nchini Namibia mwanzo mwa mwezi Septemba 2025.

Katika hatua nyingine za kuchangia matumizi ya huduma jumuishi za fedha, amesema Benki Kuu imeanzisha mazingira ya majaribio ya ubunifu (Bank of Tanzania Fintech Regulatory Sandbox Regulations, 2024) ili kuchochea wabunifu kuweza kujaribu bunifu zao.

Pia, Benki Kuu kwa kutambua umuhimu wa huduma bora umeanzisha mfumo maalumu wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi (SEMA na BoT) ili kuhakikisha kero za wananchi juu ya huduma za fedha zinashughulikiwa kwa wakati.

"Mafanikio haya ni kielelezo cha uongozi thabiti wa Benki Kuu chini ya Gavana Emmanuel Tutuba katika kusimamia juhudi za kuongeza na kuchochea matumizi ya huduma za fedha kwa kutumia teknolojia.

"Hatua hizi zinalenga kuongeza ufanisi, kupunguza gharama, na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa na kuboresha maisha yao,"amefafanua Bi.Shaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news