DCEA yakamata 940 na kilo 33,000 dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imewakamata watuhumiwa 940 wakihusishwa na tuhuma za kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ameyasema hayo leo Septemba 8,2025 ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema, watuhumiwa hao wanahusishwa katika matukio yaliyofanikisha ukamataji wa kilogramu 33,077.623 za dawa za kulevya aina mbalimbali.

Kati ya dawa hizo ambazo zimekamatwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba,2025 Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kilogramu 4,553 zilikuwa mbegu za bangi.

Pia, amebainisha kuwa,kupitia operesheni maalum iliyoendeshwa na mamlaka hiyo, wameteketeza ekari 64 za bangi.

"Na tumekamata silaha mbili za moto aina ya gobore na bastola ikiwa na risasi 11, magari tisa, bajaji mbili na pikipiki 26 zilizohusishwa kwenye uhalifu huo."
Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam katika Mtaa wa Tupendane uliopo Manzese wilayani Ubungo walikamata watu watatu akiwemo raia wa Lebanon.

Amesema, watuhumiwa hao walikuwa na kilogramu 2.443 za dawa z kulevya aina ya Cocaine.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, dawa hizo ziliingizwa nchini kutokea nchini Brazil kupitia nchini Kenya hadi Uganda na baadaye Tanzania kwa njia za vipenyo.

Katika tukio lingine amesema,jijini Dar es salaam, kwenye klabu ya “Bad London” iliyopo Temeke kwa Azizi Ally na klabu ya “Sanaa” katika eneo la “Reggae bar” iliyopo Masaki, walikamata sigara za kielektroniki (e cigarette) pisi 50 zilizotengenezwa kwa bangi zenye ujazo wa mililita 10 kila moja.
Sigara hizo za kielekroniki zilizotengenezwa kwa kutumia kemikali pamoja na skanka ziliingizwa nchini kutokea Uingereza.

Miongoni mwa Kemikali hatarishi kwenye bangi hizo ni pamoja na THC, benzene na madini ya cadmium, lead, na mekyuri.

"Kemikali hizo pamoja na madhara mengine ya kiafya, huweza kusababisha magonjwa ya akili, saratani, kuharibu mimba kwa mama wajawazito, kuathiri maendeleo ya ukuaji wa mtoto akiwa tumboni, kusababisha udumavu wa akili baada ya mtoto kuzaliwa na hivyo kuathiri uwezo wa kujifunza pamoja na uraibu."

Aidha, katika eneo la Bahari Beach amesema, walimkamata raia wa Marekani na mke wake raia wa Tanzania wakiwa na chupa 11 za dawa ya kulevya aina ya Ketamine pamoja na bangi na hatua za kisheria zinaendelea dhidi yao.

Vilevile, kupitia kampuni za usafirishaji vifurushi jijini Dar es salaam,waliwakamata watu wanne kwa kukutwa na kilogramu 10.37 za mirungi wakiwa kwenye hatua za kuisafirisha kwenda nje ya nchi huku ikiwa imefichwa kwenye vifungashio vyenye chapa ya bidhaa za chai, kwa lengo la kukwepa kubainika.

Kadhalika, kupitia mifumo ya ufuatiliaji ya kimataifa katika kuzuia uchepushwaji wa kemikali bashirifu kutumika kutengeneza dawa za kulevya,Kamishna Jenerali Lyimo amesema, walizuia uingizwaji nchini lita 69.8 za kemikali aina ya Methyl ethyl ketone (MEK) na Ephedrine ambazo zilikuwa ziingizwe hapa nchini kinyume na taratibu.

Pia,kupitia operesheni zilizofanyika mkoani Mara, tulimkamata mhalifu kinara wa uzalishaji na usafirishaji wa bangi aitwaye Masero Ryoba Muhabe (44) akiwa na tani 6.5 za bangi. Kwa muda mrefu, Muhabe amekuwa akijihusisha na uzalishaji na biashara ya bangi wilayani Tarime Mkoani Mara na kusafirisha ndani na nje ya nchi.

Katika tukio lingine mkoani humo,amesema walimkamata Simoni Gervas Mkonda (51) akiwa na kilogramu 193 za bangi pamoja na silaha aina ya bastola ikiwa na risasi 11 ambayo amekuwa akiimiliki kinyume cha sheria akiitumia kulinda biashara zake haramu.

Aidha, mkoani Mbeya,waliwakamata Henry Shao (36) na Veronika Samumba (31) wakiwa na biskuti 241 zilizotengenezwa kwa bangi.

"Watajwa ni wahandisi na wafanyakazi wa kampuni binafsi za ujenzi za HSS Engineering Company Limited na JIC Company Limited za jijini Mbeya.

"Baada ya upekuzi eneo la mtaa wa Forest watuhumiwa walikutwa na vifaa wanavyovitumia kutengeza biskuti hizo na kueleza kwamba wateja wao wakubwa ni wahandisi na vijana wa vyuo na mitaani."

Pia, mkoani Mwanza amesema walikamata watuhumiwa sita wakiwa na kilogramu 452 za dawa za kulevya aina ya bangi zikisafirishwa na gari aina ya Skania namba T 384 BWN likiwa na tela namba T.602 ANQ mali ya kampuni ya CocaCola ya NYANZA iliyopo Mwanza pamoja na bajaji mbili zilizokuwa zinabeba bangi hizo kutoka kwenye gari tajwa.

Vilevile, kupitia operesheni walizozifanya katika Mikoa ya Mara, Tabora, Kilimanjaro, Pwani, Arusha, Tanga, Ruvuma na Morogoro, walikamata kilogramu 25,919.8 za bangi, mirungi, skanka na Heroine, kilogramu 4,553 za mbegu za bangi na kuteketeza ekari 64 za mashamba ya bangi.

"Tunaendelea kuvunja mitandao ya dawa za kulevya na kubaini mbinu mpya za biashara na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo kuongeza wigo wa utoaji elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, lengo likiwa ni kuakisi dhamira ya Taifa katika kulinda usalama wa wananchi na kuimarisha uchumi, kujali utu, kulinda afya za watanzania, hatimaye kujenga jamii imara kwa ustawi wa Taifa letu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news