NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika eneo la Bahari Beach jijini Dar es Salaam imemkamata raia wa Marekani na mke wake raia wa Tanzania wakiwa na chupa 11 za dawa ya kulevya aina ya Ketamine pamoja na bangi.
Hayo yamesemwa leo Septemba 8,2025 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari ambapo hatua za kisheria zinaendelea dhidi yao.Vilevile, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kupitia kampuni za usafirishaji vifurushi jijini Dar es salaam waliwakamata watu wanne kwa kukutwa na kilogramu 10.37 za mirungi wakiwa kwenye hatua za kuisafirisha kwenda nje ya nchi
Amesema,mirungi hiyo ilikuwa imefichwa kwenye vifungashio vyenye chapa ya bidhaa za chai, kwa lengo la kukwepa kubainika.
"Kadhalika, kupitia mifumo ya ufuatiliaji ya kimataifa katika kuzuia uchepushwaji wa kemikali bashirifu kutumika kutengeneza dawa za kulevya, tulizuia uingizwaji nchini lita 69.8 za kemikali aina ya Methyl ethyl ketone (MEK) na Ephedrine ambazo zilikuwa ziingizwe hapa nchini kinyume na taratibu."Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mamlaka hiyo inaendelea kuvunja mitandao ya dawa za kulevya na kubaini mbinu mpya za biashara na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo kuongeza wigo wa utoaji elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya.
Amesema,lengo ni kuakisi dhamira ya Taifa katika kulinda usalama wa wananchi na kuimarisha uchumi, kujali utu, kulinda afya za watanzania, hatimaye kujenga jamii imara kwa ustawi wa Taifa letu.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
.jpeg)