DODOMA-Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mheshimiwa Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo ametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kukagua maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mwambegele alitembelea majimbo ya uchaguzi ya Chamwino na Mtera, ambako alipokea taarifa kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri hiyo kuhusu hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.Aidha,Jaji Mwambegele alikagua vifaa vya uchaguzi ambavyo tayari vimewasili katika Halmashauri hiyo na kutoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa ipasavyo hadi siku ya kupiga kura.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utafanyika Oktoba 29, 2025 kote nchini.Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendelea kutoa wito kwa wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Kaulimbiu ya uchaguzi mwaka huu ni "Kura Yako, Haki Yako-Jitokeze Kupiga Kura."







