Matokeo ya VACS 2024:Waziri Pembe atoa wito kwa wataalamu na wadau nchini

ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar, Mheshimiwa Riziki Pembe Juma amewataka wataalam kutumia vizuri matokeo ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na vijana uliotangazwa jana na Ofisi ya Mtakwimu wa Serikali, kwani lengo la utafiti huo ni kuchambua hali halisi ya ukatili unaotokea nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ndugu Abeida Rashid Abdallah wakiteta jambo katika kikao cha Uwasilishaji wa Matokeo Muhimu ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka (VACS 2024) kikao hicho kimefanyika jana katika ukumbi wa Madina tul bahari Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Pia matokeo hayo yanalenga kusaidia Serikali na wadau kupanga mikakati madhubuti ya kuzuia vitendo hivyo, na kuimarisha ustawi, usalama na maendeleo ya watoto na vijana.

Ameyasema hayo huko katika ukumbi wa Madina tul Bahari Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja wakati akifungua kikao cha Uwasilishaji wa Matokeo Muhimu ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka (VACS 2024).
Mhe. Riziki amewataka wataalam wote ambao wanahitaji kutumia matokeo ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na vijana ya mwaka 2024 kuyatumia vizuri bila ya kuleta athari kwa nchi na wananchi wake kwani Serekali ya Mapinduzi Zanzibar inawapenda na kuwajali wananchi wake wote ikiwa na adhma ya kuwasikiliza matatizo na changamoto zao wanazopitia.

“Naomba wataalamu mtumie vizuri matokeo ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na vijana, lengo la utafiti huu ni kuchambua hali halisi ya ukatili unaotokea nchini, ili kusaidia Serikali na wadau kupanga mikakati madhubuti ya kuzuia vitendo hivyo, kuimarisha ustawi, usalama na maendeleo ya watoto na vijana na sio kuleta athari kwa taifa letu,”amesema Mheshimiwa Riziki.
Mhe. Riziki ameleza Matokeo ya utafiti huo yamebaini kuwa ukatili wa kingono unafanana kwa wanaume na wanawake (asilimia 6%), huku ukatili wa kimwili na kihisia ukiwa mkubwa zaidi kwa wanaume (asilimia 20% na 19%) ikilinganishwa na wanawake (asilimia 9% na 11%).

Aidha Waziri huyo ameitaka jamii kuendelea kupiga na kukemea vikali vitendo hivi kwani vinarudisha taifa nyuma kwa maendeleo ya vijana, wanawake na Watoto. Pia ametowa wito kwa wazazi na walezi kuimarisha ulinzi na usalama katika familia ili kuweza kulinda mila silka na tamaduni na kuendelea kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Health Promotion Support (THPS) Dkt George Anatory amewashukuru wadau wote walioshiriki katika kazi ya Utafiti wakiwemo maafisa wa THPS pamoja na vijana waliyohojiwa katika utafiti huo. Pia shukran za dhati ziende kwa Shirika la UNICEF kwa msaada mkubwa waliyoutoa katika kuwezesha na kufanikisha VACS 2024.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ndugu Abeida Rashid Abdallah amewataka wadau wasichoke kuendelea kupinga vita vitendo vya udhalilishaji kwani matokeo hayo yatawasaidia kuweza kuongeza kasi ya kutatua changamoto zinazojitokeza.

Tangazo Rasmi la Utafiti wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024 ulifanyika Juni 9, 2025 katika hoteli ya Delta Marriot, Dar es Salaam

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news