Matumizi ya nishati ya kupikia yaongezeka nchini

DAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha.Felchesmi Mramba ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchinj yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 20.3 huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 80 ndani ya miaka 10, ambapo hadi sasa imebakia miaka tisa.
Mhandisi Mramba ameyasema hayo leo Septemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi kwa ushirikiano na Wizara ya Nishati pamoja na wadau mbalimbali likibebwa na kaulimbiu ya ‘Nishati safi ya Kupikia Okoa Maisha, Linda Mazingira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mha. Mramba amesema,“Nishati Safi ya Kupikia siyo jambo la kinadharia bali ni jambo linalohusu maisha, mazingira na uchumi huku msingi wake mkuu ukiwa ni kulinda afya, mazingira pamoja na maendeleo jumuishi.”

Aidha, Mhandisi Mramba ameendelea kuwahamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia akikumbusha kuwa, takwimu zinaonesha kuwa takribani watanzania 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua ambayo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na uvutaji wa moshi unaotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ikiwemo kuni na mkaa.

Ameeleza kuwa, kutokana na athari hizo Serikali chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034 uliozinduliwa mwezi Mei 2024 ambao utawezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia.
Sanjari na hayo, Mha. Mramba amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi ya kupikia kitaifa na kimataifa kwa Uongozi wake wa mfano na dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi, salama na nafuu ya kupikia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news