Mlipuko wa 16 wa Ebola waripotiwa nchini DRC

NA DIRAMAKINI 

JAMHURI ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeendelea kukabiliwa na milipuko mbalimbali ya magonjwa kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na mpox, kipindupindu, malaria na ebola ambayo imeibuka upya.
File: CDC photo.

Septemba 4,2025 Wizara ya Afya ya Umma ya DRC imetangaza mlipuko wa 16 wa Ugonjwa wa Virusi vya Ebola (EVD) baada ya uthibitisho wa virusi vya Ebola (EBOV), vilivyokuwa vikitambulika kama Zaïre ebolavirus.

Uthibitisho huo unakuja baada ya kipimo cha Polymerase Chain Reaction (PCR) kutoka sampuli za mgonjwa katika kituo cha afya Bulape kilichopo Mkoa wa Kasai.

Ripoti za afya zinabainisha kuwa,kujitokeza tena kwa Ebola katika maeneo ya mbali yenye upatikanaji mdogo wa huduma za afya si jambo jipya, kwani milipuko 15 ya Ebola tayari imeshatokea nchini humo hapo awali.

Mwishoni mwa Agosti, 2025 mamlaka ya afya huko Bulape, Mkoa wa Kasai ilitoa tahadhari kuhusu visa vya watu waliokuwa wakionesha dalili za homa ya kutokwa na damu pamoja na vifo vilivyohusiana, kwa wagonjwa na pia kwa wahudumu wa afya.

Aidha, kwa kuhisi ni Ebola, kipimo cha mate kutoka kwa mtu aliyefariki na sampuli tano za damu zilichukuliwa kutoka kwa wagonjwa sita waliodhaniwa kuwa na ugonjwa huo na kutumwa kwenye maabara ya Kitaifa ya Institut National de Recherche Biomédicale (INRB) huko Kinshasa kwa ajili ya vipimo na uthibitisho.

Pia, Septemba 3,2025 sampuli sita zilifanyiwa vipimo katika maabara hiyo kwa kutumia kifaa cha GeneXpert Ebola Assay, mfumo wa BioFire FilmArray System (Global Fever Panel) na PCR.

Sampuli zilizokuwa na matokeo chanya ya EBOV kupitia PCR ziliendelea kufanyiwa uchambuzi wa mlolongo wa jeni kwa kutumia kifaa cha usomaji wa jeni cha Oxford Nanopore Technology.

Taarifa hizi za karibuni kuhusu uwepo wa ugonjwa huo inaendelea kutupa angalizo Watanzania ikizingatiwa kuwa,wananchi wa Congo DRC na Tanzania wana mwingiliano wa namna mbalimbali hususani katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kuanzia mipakani na kuendelea.

Hii inatokana na ukweli kwamba,mwingiliano kati ya Tanzania na Congo DRC ni wa kihistoria, kijiografia, kijamii, na kiuchumi.

Mahusiano haya yana mchango mkubwa katika maendeleo ya kanda ya Maziwa Makuu na Afrika Mashariki kwa ujumla. Ingawa linapokuja suala la kiafya inapaswa kila mmoja achukue tahadhari ili kujiweka salama,jamii na mataifa yote kwa ujumla.(NA).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news