MANYARA-Aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Remiti kilichopo Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara,Bw.Godbless Felix Mollel amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa.
Shauri hilo la Uhujumu Uchumi namba 22415/2025 limefunguliwa Septemba 15,2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Mheshimiwa Onesmo Nicodemo.
Mshtakiwa anashtakiwa kwa makosa ya ufujaji na ubadhirifu Kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 R. E 2022, kikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na pamoja ya kupanga Sura ya 200 R:E 2022.
Aidha,mshtakiwa anashtakiwa kwa kosa la wizi akiwa mtumishi wa umma kinyume na vifungu 258 na 270 vya Kanuni za Adhabu (sura ya 16 R.E 2022).
Akisoma hati ya mashtaka Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Faustin Mushi amesema, mshtakiwa wakati akitekeleza majukumu yake ya Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Remit alifanyia ubadhirifu wa fedha za kijiji shilingi 3,300,000 ambazo zilikuwa chini yake,kutokana na nafasi yake.
Mshtakiwa amekana kutenda makosa yote yanayomkabili na shauri limehairishwa hadi Septemba 25,2025 kwa ajili ya kusikilizwa hoja za awali (PH).
Kwa sasa mtuhumiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao wote wamesaini bondi ya shilingi 2,000,000 kila mmoja.
.jpeg)