Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yawataka wahariri kutumia kalamu zao kudumisha amani,umoja na mshikamano nchini

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini kuzingatia maadili na kutumia kalamu zao kwa uadilifu katika kuhabarisha umma ili kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Ni kwa kuangazia umuhimu wa kulinda amani, kudumisha umoja,mshikamano na usalama wa taifa wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.Ipyana Mlilo wakati akifunga kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wahariri wa vyombo vya habari, kilichofanyika leo Septemba 12,2025 jijini Dodoma.

Amesema kuwa,Sekta ya Habari ni muhimu katika taifa, hivyo kupitia kikao hicho kimetoa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri ili kufanikisha utoaji wa elimu kwa jamii kwa weledi.

“Kikao kazi hiki kimekuwa na manufaa makubwa katika kuhakikisha jamii inapata uelewa mpana kuhusu masuala ya kisheria. Tumejadiliana mambo mengi na yote yamepokelewa kwa uzito,tutayafanyia kazi kwa lengo la kuendelea kuelimisha umma," amesema Bw.Mlilo.

Awali,akielezea majukumu ya Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) katika kikao kazi hicho Rais wa chama hicho, Bw.Bavoo Junus amesema kuwa,TPBA ni nguzo muhimu katika kulinda,kusimamia na kutetea maslahi ya taifa na rasilimali zake.

Ameeleza kuwa,TPBA ni chama cha kitaaluma kinachowaunganisha wanasheria wote wanaohudumu katika ofisi za umma ikiwemo halmashauri, wizara, wakala, taasisi za serikali, na kampuni ambazo Serikali ina hisa.

“Tuna jukumu la kuelimisha jamii kuhusu masuala ya sheria. Hili limefanikiwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ambayo imetekelezwa kwa mafanikio makubwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Bw. Junus.

Amefafanua kuwa TPBA, kupitia umoja wake, imeunda jukwaa la kuwaunganisha mawakili wa serikali ambapo wamekuwa wakijadiliana kuhusu taaluma zao, pamoja na kutetea maslahi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikao kazi hicho ambacho kimehitimishwa leo kimefunguliwa Septemba 11,2025 na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.Samwel Maneno ambapo amebainisha kuwa, ofisi hiyo itahakikisha inaendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kutunga sheria ambazo zinalinda haki na utu wa mtu.

Vilevile, umoja wa kitaifa, demokrasia na kuchochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni sehemu ya utekekezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Amesema kuwa, vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhakikisha jamii inapata habari sahihi kutoka kwenye vyanzo sahihi na kwa wakati sahihi ambapo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni sehemu sahihi ya kupata taarifa zote zinazohusiana na sheria nchini.

“Habari mnazoziandika zinahamasisha umoja na mshikamano kuendelea kuwepo nchini? Mkilitambua hilo ndiyo mtaweza kufahamu ni habari gani jamii ina kiu ya kuisikia kuhusu yale ambayo yanafanywa na Serikali na yale ambayo yako kwa mujibu wa sheria.

"Sanjari na yale ambayo wananchi wanapaswa kuyafanya kama wajibu wao na yale ambayo ni haki yao pia ya kisheria,”alisisitiza Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Pia, amesema katika mwaka uliopita wa fedha ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo kufanikiwa kuandaa miswada 19 ya kisheria pia imetafsiri sheria 433 kati ya 446 zilizopo hapa nchini kutoka kwenye lugha ya Kiingereza kwenda kwenye lugha rahisi ya Kishwahili.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwapa wananchi uwanda mpana wa kuzisoma sheria hizo na kuzielewa ili kutambua umuhimu wa utii wa sheria bila shuruti.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema, tafsiri za sheria 13 zilizosalia inaendelea na ofisi hiyo itaendelea kuwajengea wananchi uwezo zaidi wa kuzifahamu sheria hizo.

Katika hatua nyingine amesema,wamefanikisha maazimio mawili katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na urekebu wa sheria 466 nchini ambapo kwa sasa zimeshazinduliwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na zinafanya kazi.

Aidha ofisi hiyo imefanikisha upekuzi wa mikataba 3,446 ya kitaifa na kimataifa ambayo inahusisha ununuzi,ujenzi,ukarabati na utoaji wa huduma za jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news