PBA yaitaka TLS kuheshimu wajibu wa kisheria kwa wananchi

NA GODFREY NNKO

CHAMA cha Mawakili wa Serikali (PBA) kimelaani maazimio ya Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria (TLS) kuhusu tukio lililotokea Septemba 15,2025, kikisema kwamba baadhi ya maamuzi ya TLS yanakiuka Katiba, sheria za nchi na misingi ya taaluma ya uwakili.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA),Wakili Addo November leo Septemba 23,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

PBA kimeanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 16A (1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura 268 na Tangazo la Serikali Na.589 la Agosti 16,2019.

"Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inasema ...kila mtu ana wajibu wa kutii Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano.”

"TLS, kama taasisi ya kisheria na legal person, ina wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha kwamba maamuzi yake hayapingani na sheria iliyoianzisha (TLS Act) na sheria nyingine husika kama Legal Aid Act."

Amesema, TLS kama chama cha kitaaluma kilichoanzishwa kisheria kwa mujibu wa Tanganyika Law Society Act, kina wajibu wa kuhakikisha maadili, heshima na weledi vinaendelezwa ndani ya taaluma ya uwakili.

Aidha,amekumbusha kuwa kila wakili aliyeandikishwa ni mwanachama wa lazima wa TLS, wakiwemo mawakili wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Kauli au maazimio ya TLS yanayolenga kuzuia mawakili wasitoe msaada wa kisheria ni kinyume na wajibu wa msingi wa wakili kama afisa wa Mahakama,” amesema Wakili November.

PBA imesisitiza kuwa, utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi ni wajibu wa kisheria, si hiari, kwa mujibu wa Legal Aid Act [Cap. 21 R.E. 2019].
Pia,amesema kwamba hatua yoyote ya kusitisha huduma hizo kwa wananchi wa kipato cha chini ni kitendo kinachokiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan Ibara ya 13(1) inayohakikisha usawa mbele ya sheria.

"TLS haina mamlaka ya pekee ya kushughulikia nidhamu za mawakili, kwani kwa mujibu wa Advocates Act [Cap. 341], nidhamu ya mawakili inasimamiwa na Kamati ya Nidhamu ya Mawakili inayojumuisha Jaji wa Mahakama Kuu, Mkurugenzi wa Mashtaka, na mwanachama mmoja wa TLS.

“Tunashauri kwa heshima viongozi wa TLS kuzingatia wajibu wao wa kisheria na kitaaluma, na kuepuka maamuzi yanayoweza kuathiri haki za wananchi na heshima ya taaluma ya uwakili,”amesema Wakili November.

Vilevile amesema,taasisi zote za kitaaluma zinapaswa kushirikiana kwa weledi katika kulinda misingi ya haki, usawa, na utawala wa sheria, badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuzorotesha huduma za kisheria kwa wananchi wa kawaida nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news