Rais Dkt.Samia na Mkakati wa Kidiplomasia kupitia Utalii,Royal Tour yazidi kuvutia Dunia

NA GODFREY NNKO

FILAMU ya kihistoria ya Royal Tour iliyoandaliwa mwaka 2021/2022 kwa lengo la kuitangaza Tanzania kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na mtangazaji maarufu wa Marekani, Peter Greenberg imeendelea kuifanya Sekta ya Utalii kuwa na mafanikio zaidi.
Rais Dkt.Samia ndiye mhusika mkuu katika filamu hiyo, hatua ambayo haijawahi kufanywa na kiongozi mwingine yeyote wa Afrika Mashariki.

Kupitia Royal Tour, Rais Dkt.Samia alichukua jukumu la kuitangaza Tanzania kama kivutio kikuu cha utalii barani Afrika kwa kuonesha vivutio vya asili, urithi wa kihistoria, tamaduni za watu wake na mazingira salama ya uwekezaji.

Hatua hiyo ilichagizwa na ukweli kuwa, Tanzania, ni Taifa lenye ardhi bora, vivutio vya kipekee, mila na maisha ya kusisimua, ni moja ya nchi zinazoangaza barani Afrika na kuonekana ulimwenguni kote kwa uzuri wake, utofauti wake na nafasi zake za kipekee.

Miongoni mwa mambo kadhaa yanayoifanya Tanzania kusimama tofauti na kuwa na heshima ya kimataifa ni pamoja na mali asili za kipekee kuanzia hifadhi za wanyamapori na mbuga za Taifa.

Ukienda mfano kule Serengeti, Ngorongoro, Selous au Mwalimu Nyerere, Ruaha na kwingineko utaona namna mbuga hizi zinavyowavutia watalii wengi kwa kuona wanyama wa kila aina na mandhari ya asili ambayo si rahisi kuipata mahali pengine.

Kwa hiyo, hifadhi za taifa za Tanzania ni hazina ya asili na utamaduni ambazo zinatoa fursa nyingi za utalii. Kila hifadhi ina uzuri wake wa kipekee, ikiwa na mazingira tofauti, wanyama wa porini, na tamaduni tofauti za wenyeji.

Vilevile, Tanzania ina milima ya kupendeza na mazingira ya kuvutia ikiwemo Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu zaidi barani Afrika pamoja na milima mingine yenye barafu, maeneo ya misitu na mito ambayo inaongeza ufanisi wa mazingira ya kipekee.

Pia, kuna Pwani nzuri na Bahari ya Hindi ambapo Zanzibar, Mafia, Pemba kuna visiwa na fukwe safi zenye matumbawe, maji ya kuvutia kwa utalii, uvuvi na utamaduni wa pwani unaochanganya historia ya Bahari ya Hindi na tamaduni za Kiislamu na Kiafrika.

Aidha, kuna urithi wa kihistoria kuanzia Mji wa Bagamoyo, Zanzibar Stone Town, historia ya biashara ya ukoloni na ya utumwa, pia urithi wa kale.

Bila kusahau, maonesho ya sanaa, ngoma, matamasha ya kitamaduni yakitoa sura ya kipekee ambayo watu wengi duniani wanapenda kugundua, kushiriki na kuhamasishwa nayo.

Kutokana na wingi wa maliasili hizo, Tanzania ina sera na mikakati ya kulinda ekolojia na maeneo ya ulinzi wa wanyama, kupunguza athari za binadamu na kuongeza manufaa kwa jamii za karibu.

Watalii wa sasa wanathamini zaidi utalii unaojali mazingira, na Tanzania ipo juu katika utoaji wa uzoefu huo.

Tanzania sio tu nchi yenye maliasili tajiri na uzuri wa kuvutia, lakini pia ina uwezo mkubwa wa kuyachangamsha hayo kwa manufaa ya taifa na ulimwengu.

Imekuwa ikijitolea kuhakikisha kwamba maendeleo, utalii, utamaduni na maliasili vinavyopatikana vinatunzwa kwa vizazi vijavyo.

Uwekezaji unaingia, watalii wanafurahi na jamii zinapokea manufaa ya moja kwa moja, ndiyo maana ikiwa Dunia inatafuta mahali ambapo utajiri wa asili unachanganywa na utamaduni wa kuvutia, utulivu wa kisiasa, fursa za biashara, na uzoefu wa kipekee wa watu, Tanzania ni chagup namba moja na fahari ya kuvutia.

Ndiyo maana chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeendelea kuonesha uwezo mkubwa wa kimataifa kwa mafanikio makubwa katika sekta ya utalii na ufugaji wa nyuki, ikiweka historia mpya katika maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani na kupata tuzo ya Dhahabu ya Apimondia.

Katika kilele cha maadhimisho hayo mwaka huu 2025, yaliyofanyika katika eneo la picnic la Hifadhi ya Ngorongoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas ametangaza kwamba, Tanzania imetajwa na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kuwa nchi inayoongoza Afrika kwa ongezeko kubwa la idadi ya watalii baada ya janga la UVIKO-19.

“Kwa mujibu wa ripoti ya UN Tourism ya 2024, Tanzania imekuwa na ukuaji wa asilimia 48 ya watalii wa kimataifa, ikiwa mbele ya Ethiopia asilimia 40, Morocco asilimia 35, Kenya asilimia 11 na Tunisia asilimia 9,” amesema Dkt.Abbasi.

Aidha, ripoti ya mwaka 2025 imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 20 bora duniani zinazofanya vizuri katika sekta ya utalii, kwa wastani wa ukuaji wa zaidi ya asilimia 50.

Takwimu Zinazovutia

Dkt.Abbasi ameeleza kuwa, idadi ya watalii wa kimataifa ilipanda kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi 2,141,895 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 132.1. Watalii wa ndani nao waliongezeka kutoka 788,933 hadi 3,218,352, ongezeko la asilimia 307.9.

Kwa ujumla, watalii wa ndani na nje walifikia milioni 5.36 kufikia Desemba, 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 107.2 ikilinganishwa na mwaka 2021.

Vilevile, mapato kutoka sekta ya utalii yaliongezeka kutoka dola bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi bilioni 3.9 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 200.

Haya ni mafanikio yanayoendana na malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020/2025, inayolenga kufikia watalii milioni 5 na mapato ya dola bilioni 6 ifikapo mwaka huu wa 2025.

Katika kipindi cha Januari hadi Julai 2025 pekee, Tanzania ilipokea watalii milioni 1.27, ongezeko la asilimia 9.2 kutoka milioni 1.16 mwaka 2024.

Pongezi 

Dkt.Abbasi ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa za kuinua sekta ya utalii kupitia uboreshaji wa miundombinu ya utalii,matumizi ya TEHAMA na mifumo ya kidijitali.

Aidha, filamu za kimataifa kama The Royal Tour na Amazing Tanzania, zilizoongeza utangazaji wa nchi duniani kote.

Tanzania pia imepokea tuzo mbalimbali kutoka World Travel Awards (WTA), zikiwemo za Eneo Bora kwa Safari Afrika, jambo linaloendelea kuimarisha nafasi ya nchi katika ramani ya utalii duniani.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ya “Utalii na Mabadiliko Endelevu” imeweka mkazo kwenye ubunifu, ushirikishwaji wa jamii na maendeleo ya biashara endelevu katika ukuaji wa sekta hiyo muhimu.

Sekta ya Nyuki

Wakati huo huo, Tanzania mwaka huu wa 2025 imepata heshima kubwa kimataifa baada ya kutwaa Medali ya Dhahabu katika Kongresi ya 49 ya Apimondia, iliyofanyika katika Ukanda wa Scandinavia barani Ulaya.

Katika kipengele cha "Large Stand" (zaidi ya mita 36 za mraba), banda la Tanzania lilishinda kwa ubunifu, mpangilio wa kitaalamu na ubora wa maonesho ya mazao ya nyuki yaliyowavutia wageni kutoka kote duniani.

Cheti cha ushindi kilikabidhiwa na Rais wa Shirikisho la Apimondia, Jeff Pettis kama ishara ya kutambua mchango mkubwa wa Tanzania katika kukuza tasnia ya nyuki duniani.

“Ushindi huu unathibitisha kuwa Tanzania ni kitovu kinachochipukia kwa uzalishaji na usindikaji wa mazao ya nyuki duniani,”amesema Hussein Msuya, Kamishna Msaidizi wa Rasilimali za Nyuki.

Maonesho hayo yalijumuisha bidhaa mbalimbali kama asali ya Tanzania, chavua, nta na bidhaa za vipodozi, ambazo ziliwasilishwa na wakulima, wajasiriamali na taasisi mbalimbali kutoka nchini.

Ushindi huo unatarajiwa kuongeza thamani ya bidhaa za nyuki katika masoko ya kimataifa, na kuwainua wakulima wadogo kupitia mapato zaidi na ajira mpya.

Mbali na hayo,Dkt.Abbasi na maafisa wengine wanasisitiza kuwa, mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za utafiti na wananchi, hasa wale wanaoishi karibu na hifadhi, misitu na maeneo ya uzalishaji wa nyuki.

Aidha, amewahimiza Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za utalii na ufugaji wa nyuki, kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Utalii ya 1999 na Sheria ya Utalii Sura ya 65, pamoja na miongozo ya tasnia ya misitu na nyuki.

Mafanikio haya ya kimataifa yanaendelea kuonesha kuwa, Tanzania ni nchi yenye uwezo mkubwa wa kutumia rasilimali asilia kwa njia endelevu na jumuishi.

Kupitia uongozi wa kisasa, uwekezaji katika teknolojia na ubunifu wa sekta binafsi, Tanzania sasa imejipambanua kama kinara wa utalii Afrika, bingwa wa ubora katika bidhaa za nyuki duniani na Taifa linaloongoza katika diplomasia ya kiuchumi na mazingira.

Tanzania si tu kivutio cha watalii, bali pia ni nguzo ya maendeleo ya kijani barani Afrika mahali ambapo utalii, uhifadhi na uchumi vinaishi kwa pamoja.

Rais Dkt.Samia amekuwa akihimiza Watanzania kujivunia vivutio vyao na kushiriki kikamilifu katika kukuza utalii wa ndani.

“Utalii si wa wageni pekee. Watanzania nao wanapaswa kushiriki katika kutembelea vivutio vyao.Hii inasaidia kuongeza mapato na kutangaza utamaduni wetu,”alisisitiza Rais Dkt.Samia wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo jijini New York.

The Royal Tour ya Rais Dkt.Samia ni hatua ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa katika sekta ya utalii Tanzania.

Aidha, imesaidia kuionesha Tanzania kwa macho ya Dunia na kuongeza hamasa ya maendeleo katika sekta hiyo muhimu ya uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news