NA LWAGA MWAMBANDE
UKIREJEA katika maandiko matakatifu, utaona kuwa mtumishi wa Mungu,Ayubu pamoja na kupitia majaribu mazito ya kupoteza kila kitu chake ikiwemo heshima, familia na mali zake, hakuacha kumwabudu Mungu na hakuthubutu kumtenda Mungu dhambi.
Kwani,aliendelea kusimama imara, rejea Ayubu 19:25 neno la Mungu linasema,"Lakini mimi najua ya kuwa mteteaji wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi."
Vivyo hivyo, Paulo na Sila hawakuacha kumsifu na kumwomba Mungu pamoja na kwamba walipigwa na kufungwa gerezani.
Na hata walipotoka gerezani hawakuacha kumtumikia Mungu, waliendelea kumtumikia Mungu hadi pumzi yao ya mwisho.
Naye Yusufu hakuacha kumwamini Mungu wake hata baada ya kuumizwa na ndugu zake kwa kutaka kumwua na kisha kumuuza utumwani.
Yusufu, hata akiwa kwenye nchi ya utumwa aliendelea kumwamini Mungu wake na kuishi katika mwongozo wake bila kukata tamaa.
Kwa msingi huo,mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anaendelea kusisitiza kuwa,tunapaswa kumwamini na kumwabudu Mungu, kwani Mungu ndiye kila kitu. Endelea;
1. Kuna neno gani gumu, Mungu asililoweza,
Yeye peke anadumu, kwamba yote anaweza,
Yale tusiyofahamu, Mungu anatekeleza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
2. Sara na wake utasa, Mungu aliumaliza,
Katika uzee hasa, kuzaa asipoweza,
Kwa Neno siyo siasa, unyonge aliutweza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
3. Ahadi ya kwake Mungu, Ibrahimu katimiza,
Watu mafungumafungu, jinsi aliwaongeza,
Nasi tuko kwenye fungu, uzao tunakoleza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
4. Kwa Eliya na Baali, mabishano kutokeza,
Yupi ni Mungu halali, sadaka kuteketeza,
Manabii wa Baali, wengi walijitokeza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
5. Wakaita Mungu wao, sadaka kuteketeza,
Kujikatakata kwao, moto haukutokeza,
Siku nzima ile yao, na wala hawakuweza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
6. Na ijulikanaye leo, Eliya akatangaza,
Mungu mwenye matokeo, awezaye teketekeza,
Ule wa Mungu upeo, pale ukajitokeza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
7. Mungu tunayemjali, sadaka liteketeza,
Lishusha moto mkali, kulamba kuvimaliza,
Siyo hivyo kwa Baali, muda bure lipoteza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
8. Simba liwafumba vinywa, Dany hawakummeza,
Hatari ile kaponywa, huu wa Mungu uweza,
Simba lifungua vinywa, watesi kuwamaliza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
9. Wale vijana watatu, walitaka kuwaliza,
Kwa moto siyo kifutu, waweze wateketeza,
Kuwatupia ndani tu, wa nne kaongezeka,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
10. Moto haukuwadhuru, watesi liwachakaza,
Wao na ya kwao nuru, vizuri wakatokeza,
Moto ule wa tanuru, katu haukuwaweza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
11. Tumwangalie na Musa, Farao livyomuweza,
Kutupa fimbo ya Musa, nyoka akajitokeza,
Farao kajitikisa, kwamba na yeye aweza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
12. Wachawi wake kufika, fimbo zao kuzilaza,
Ni nyoka waligeuka, kama Musa utawaza,
Ila kilichowafika, Mungu aliwachakaza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
13. Fimbo ya nyoka wa Musa, nyoka wao liwameza,
Fimbo zao walikosa, Mungu alivyowaliza,
Kumshika nyoka Musa, fimbo ikajitokeza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
14. Vipi Bahari ya Shamu, ule wa Mungu uweza,
Farao alivyodumu, kutaka kuwakata,
Na Mungu akahudumu, wapendwa wakakatiza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
15. Bahari kugawanyika, nchi kavu kutokeza,
Mahali pakapitika, ng’ambo ile kuiweza,
Maadui kuingia, wote kawaangamiza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
16. Mwanamke Msamaria, Yesu aliyomweleza,
Nani aliyajulia, au hata kuyawaza,
Mungu kumkimbilia, sisi vema kukuwaza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
17. Yule alitokwa damu, afya yake kuchakaza,
Kupona ya kwake hamu, sanasana aliwaza,
Akajitoa fahamu, kusaka ule uweza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
18. Kugusa pindo la nguo, ule wa Mungu uweza,
Ukawa ni ufunguo, teso lile kumaliza,
Nani kwetu ni chaguo, tupasaye mtukuza?
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
19. Ona uumbaji wake, Mungu yote anaweza,
Kwa huo ujuzi wake, nchi mbingu zatokeza,
Hajaweka nguzo, yake, anga linavyotokeza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
20. Kwenye uumbaji wake, Yesu anajitokeza,
Kule kuzaliwa kwake, si binadamu kuweza,
Ni zenyewe nguvu zake, alipata jitokeza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
21. Na yale maisha yake, Mungu yanamtukuza,
Kufa kufufuka kwake, nani mwingine kaweza?
Na tena kurudi kwake, jinsi atakavyotokeza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
22. Mungu kimbilio letu, kwa vile yote aweza,
Yeye ni Muumba wetu, maishani atutunza,
Na sisi imani zetu, tuweke kwake Muweza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
23. Imani kwingine kote, ni muda kuupoteza,
Viache vipite vyote, wala visije kuchuuza,
Upate dunia yote, umilele kupoteza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
24. Utukuzwe Mungu wetu, kwa vile yote waweza,
Na sisi tu wako watu, kwako ndiko twajilaza,
Hapo hatujali kitu, hakuna cha kutuweza,
Tumwamini tumwabudu, Mungu ndiye kila kitu.
(Mwanzo 18:14, Yeremia 32:17, Zekaria 8:6, Wafilipi 4:13, Warumi 8:31)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
.jpeg)