NA LWAGA MWAMBANDE
IKUMBUKWE kuwa, kumuinua Mungu ni kumtukuza, kumsifu na kumweka juu ya kila kitu katika maisha yetu.
Aidha, kama wana wa Mungu,tunapaswa kumuinua Mungu kila siku kwa sababu yeye ndiye muumba wetu na anatupenda bila masharti.
Pia,Mungu ni Mtakatifu na mwenye nguvu zote. Anastahili sifa na utukufu. Vilevile kumuinua Mungu, ni njia ya kumshukuru kwa uhai, afya, familia,wokovu na kila kitu kupitia Yesu Kristo.
Kuna njia nyingi za kumuinua Mungu kwa vitendo ikiwemo kuimba nyimbo za sifa na kuabudu,kusali na kumshukuru kila siku.
Vilevile,kumtii Mungu kwa kuishi maisha ya uadilifu,kuwapenda na kuwasaidia wengine ikiwemo kushiriki Neno la Mungu na marafiki.
Kumuinua Mungu si jambo la kanisani tu, badala yake ni mtindo wa maisha,kwani tunapomuinua Mungu hata katika kila njanya ni wazi maisha yetu yanakuwa baraka kwa wengine.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,usisubiri majibu,wewe endelea kumuinua Mungu.Endelea;
1. Sura ya kumi na mbili, Mwanzo kitabu fahamu,
Hili tunalijadili, linamhusu Ibrahamu,
Imani yenye adili, kwake Mungu ilidumu,
Usisubiri majibu,wewe umwinue Mungu.
2.Kweli aliahidiwa, hili tunalifahamu,
Baraka atapatiwa, uzazi utaodumu,
Kwenye nchi utatawa, kuzidi hata karamu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
3.Kwamba atakuwa baba, wa dunia Ibrahimu
Uzao wake tabeba, baraka za kujikimu,
Umiliki siyo haba, ardhi kubwa ya kudumu,
Usisubiri majibu,wewe umwinue Mungu.
4.Ibrahimu hakungoja, ahadi zile zitimu,
Akaona njema hoja, Mungu wake kumweshimu,
Madhabahu yake hoja, kasimika ikadumu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
5.Hapo mke wake tasa, hali yake Ibrahimu,
Hiyo haikutikisa, imani ya Ibrahimu,
Aliitumia fursa, Mungu akamheshimu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
6.Hili ni fundisho kwetu, tuishio binadamu,
Tukimwomba Mungu wetu, asikia tufahamu,
Wala tusingoje kitu, kumshukuru tudumu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
7.Pale unapomweshimu, imani yako yadumu,
Na yeye anafahamu, wampenda mwanadamu,
Shidazo atakukimu, ufurahie kwa zamu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
8.Ona sasa matokeo, imani ya Ibrahimu,
Anatajwa hadi leo, hili tunalifahamu,
Imani kubwa upeo, tujifunze wanadamu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
9.Mungu tunakushukuru, kupitia Ibrahimu,
Nasi tunapata nuru, tukiomba twafahamu,
Madhabahu kwa uhuru, kuzisimika tudumu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
10.Kama hujatenda leo, hilo tunalifahamu,
Wema wako wa upeo, inakuja yetu zamu,
Tutaona matokeo, hata tufanye karamu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
11.Ahadi za Mungu wetu, hizo kweli zinadumu,
Akikuambia kitu, kitatimia fahamu,
Kwa hiyo wajibu wetu, kumtukuza adumu,
Usisubiri majibu, wewe umwinue Mungu.
(Mwanzo 12:7-8)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
