Serikali itaendelea kuwawezesha vijana waweze kujiajiri na kuajirika-Waziri Pembe

ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar,Mheshimiwa Riziki Pembe Juma amesema, Serikali itaendelea kuwawezesha vijana katika kuhakikisha wanapata elimu itakayowawezesha kujiajiri na kuajirika.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akimkabidhi ndugu Shahira Abdallah Mohamed cheti cha mafunzo ya kupamba uso (Makeup),hafla hiyo imefanyika jana katika Ukumbi wa Baytul Yamiin,Unguja.

Mheshimiwa Pembe ameyasema hayo jana wakati akifunga mafuzo ya upambaji uso (make up) katika Ukumbi wa Baytul Yamiin Bwawani mini Unguja.

Amesema,Serikali imeamua kufanya hivyo ili kuhakikisha vijana wanapata fursa za kujiendeleza kimaisha pamoja na kudumisha utamaduni wa Zanzibar.

Waziri Pembe amesema, Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi imekuwa ikifanya jitihada za kutosha za kuinua kiwango cha ajira kwa vijana katika sekta mbalimbali zisizo rasmi kutokana na uhaba wa fursa katika sekta zilizo rasmi.
Amesema,jukumu hilo imekuwa likitekelezwa kwa vitendo kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao wandandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na SEBEP.

Mhe. Riziki amewapongeza kwa juhudi na kuwa na wazo zuri la kuandaa mafunzo hayo ya kuwawezesha vijana wa kike katika kuwasaidia kuweza kujiajiri na kuajiri kwa lengo la kuondokana na utegemezi.

"Mtaji wa kwanza wa taifa letu ni watu wake, hivyo mkono wenye ujuzi sio tena kuombaomba, bali ni kuweza kujikimu na kuchangia kuendeleza familia na taifa," amesema Mhe. Riziki.

Hata hivyo, Mhe. Riziki amewataka vijana hao kutumia vyema ujuzi walioupata si kwa kujipatia riziki pekee, bali pia kuwa mwanga katika jamii kwa kuwafundisha wengine, kuwa mfano wa uadilifu katika biashara yao, na kuwapa heshima wateja wao.
Pia, Mhe. Riziki ametumia fursa hiyo kuwahimiza vijana kuendelea kudumisha amani na usalama wakati huu wanapoelekea katika uchaguzi, wakati wa uchaguzi, na baada ya uchaguzi, ili kuhakikisha kila mmoja anaendelea kufanya pirika zake za kujipatia kipato.

Naye Mkurugenzi wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Bw. Juma Burhani Muhammed amesema, watahakikisha wanazishawishi taasisi mbalimbali kuweza kuwapatia nafasi za ajira vijana waliopatiwa mafunzo hayo ili kuendeleza ujuzi walioupata.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Kuwajengea Uwezo Vijana Kujiajiri na Kuajirika katika Uchumi wa Buluu (SEBEP), Bw. Salum Mkubwa Abdullah amesema, lengo la mradi huo ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi utakaowasaidia kuinuka kiuchumi.
Washiriki wa mafunzo hayo, katika risala yao, wamesema watahakikisha wanayafanyia kazi mafunzo waliyoyapata kwa kujiajiri na kuchangamkia fursa za ajira zilizopo nchini, huku wakimshukuru na kumpogeza mwalimu wao, ndugu Emy Broun, kwa kuwapa mafunzo hayo yatakayowasaidia kujiari na kuajiriwa.

Jumla ya vijana wanawake 52 wamepatiwa mafunzo ya upambaji wa uso (make-up) yaliyoandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi chini ya mradi wa SEBEP. Kati yao, vijana 10 wamepatiwa ajira na mwalimu wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news