Serikali kuendelea kuimarisha huduma ya maji Karatu na Monduli

ARUSHA-Hapa nchini moja ya wilaya zinazoongoza kwa biashara ya utalii na kazi za kilimo ni wilaya za Karatu na Monduli. Kwa kazi hizi, huduma ya maji ndio injini ya mafanikio zaidi kwa biashara na wananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri akiwa katika ukaguzi wa miradi ya maji wilayani Monduli. 

Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi kwa wakati katika makazi yao. Mradi wa thamani ya Shilingi bilioni 20.3 unatekelezwa na utanufaisha mji wa Monduli na wananchi katika vijiji 13.

Karatu, kwa uchache ni lango la Hifadhi ya Ngorongoro na Ziwa Manyara, pamoja na hilo imeshamiri kwa mashamba na biashara. 

Kwa Monduli, imebeba urithi wa tamaduni za kabila la Kimasai na mandhari za kuvutia, imekuwa kivutio cha wageni wa ndani ya nchi na nje ya nchi ikiwamo kivutio cha Engaruka.

Shughuli hizi zinazoingiza kipato na kuwaletea wananchi mafanikio zaidi kiuchumi zinahitaji huduma ya maji ya kutosha ili kuwa bora na kuleta matunda zaidi kwa Watanzania. 

Fursa zote hizi na kutimiza ndoto za maelfu ya wananchi, mazingira yake yanatengenezwa na Serikali.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, akiwa katika wilaya hizo mbili kikazi, ametoa majawabu na mustakabali wa Sekta ya Maji na kuimarisha huduma ya maji katika wilaya hizo.

Kazi iliyofanywa na Mhandisi Mwajuma ni safari ya kugusa maisha ya wananchi na kusikiliza sauti zao moja kwa moja. 

Katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa alikagua na kuona visima vilivyokauka, akawasikiliza akina mama ambao wanategema huduma ya maji kwa kazi mbalimbali na kuketi na viongozi wa wilaya kujadili suluhu ya kudumu.

Akiwa Wilayani Karatu Mhandisi Mwajuma alibaini changamoto ikiwemo hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 66 ikiwa pamoja na mgao wa huduma ya maji.

Pamoja na hilo, ubovu wa pampu ya kusukuma maji katika Kijiji cha Kansay. Hali hiyo ikiwafanya wateja kutumia mwendo wa ziada kutafuta huduma. Mhandisi Mwajuma baada ya kujionea hali hiyo akaamua kuweka wazi mpango wa hatua za muda mfupi, wa kati na mrefu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo hayo.

Kwa hatua ya muda mfupi, alielekeza kuwa Wataalam wa Wizara ya Maji kufanyia kazi kisima cha Bwawani mara moja ili kifanye kazi. Umamuzi huo ulifikiwa kwakuwa Kisima hicho ambacho hakijatumika kwa muda mrefu kutoa huduma kwa jamii. 

Hatua hiyo matokeo yake ni kuleta afueni kwa wananchi kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 66 ya sasa hadi kufikia asilimia 77.

Aidha, changamoto ya kuungua kwa pampu ya maji katika Kijiji cha Kansay iliyosababisha huduma kutoimarika, Mhandisi Mwajuma alitumia wasaa huo kuwathibitishia wananchi kuwa taratibu za kupata pampu mpya zipo hatua za mwisho na muda si mrefu pampu mpya itafungwa na huduma kurejea, akibainisha kwamba Serikali haiwezi kuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma muhimu ya majisafi katika makazi yao.

Kwa hatua ya muda wa kati, Mhandisi Mwajuma alielekeza Watalaam wa Bodi ya Maji, Bonde la Pangani kufanya kazi ya utafiti wa vyanzo vya maji ardhini ili kuweza kuchimba visima vingine vipya ili kuongeza uzalishaji wa maji na kuondoa utegemezi wa visima vichache vilivyopo. 

Akiongea na wananchi alisema kuwa Serikali inaliona tatizo la maji katika mji wa Karatu kama la kipaumbele, na hatua za haraka zinaendelea kuchukuliwa ili kumaliza na kuondosha uhaba unaojitokeza.

Upande wa hatua ya muda mrefu katika kupata Suluhu ya maji, Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma alisema, Wizara ya Maji itafanya utafiti wa vyanzo vya maji vya uhakika sambamba na maandalizi ya usanifu wa mradi mkubwa ambao utaimarisha huduma ya maji katika Wilaya ya Karatu kwa miaka mingi ijayo. 

Akisisitiza dhamira ya Serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini mwishoni mwa mwaka 2025.

Wilayani Monduli, mkoa wa Arusha Mhandisi Mwajuma Waziri akiwa katika eneo la Nanja-Mti Mmoja, alijumuika na wananchi kushuhudia hatua za awali za mradi mkubwa unaoendelea kutekelezwa wenye thamani ya shilingi Bilioni 20.3.

Mkandarasi Jandu Plumbers kutoka India, anatekeleza mradi huo ambao utapeleka huduma ya maji katika Mji wa Monduli na vijiji 13 vya jirani ambavyo havijawahi kupata maji ya bomba tangu wakati wa za uhuru, na mradi huo ukienda kunufaisha zaidi ya wananchi elfu 57.

Kukamilika kwa mradi huo wa kimkakati kutanufaisha Mji wa Monduli pamoja na vijiji 13 vya Wilaya hiyo ambavyo ni Maserani Juu, Meserani Bwawani, Arkatani, Lashaine, Arkaria, Mti Mmoja, Nanja, Lepruko, Losiminori, Mugumu, Eng’aroji, Naalarami, Engorika na Lengiloriti.

Idadi ya Vijiji hivi 13 kwa muda mrefu havikuwahi kufikiwa na mtandao na huduma ya majisafi tangu kupatikana kwa uhuru, hali iliyowalazimisha wananchi kutumia muda mwingi, ikiwamo kina mama na kufuata huduma ya maji nje na makazi yao hivyo kutumia muda mwingi.

Mhandisi Mwajuma alieleza kuwa Serikali imeamua kuwekeza katika mradi huo mkubwa kutokana na kipaumbele chake kwa wananchi. Alisisitiza kuwa Serikali inaufuatilia kwa karibu utekelezaji wake ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na unaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Alimuelekeza Mkandarasi kampuni ya Jandu kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo kwa mtiririko kuanzia katika chanzo kwenda kwenye maeneo husika ili uanze kutoa huduma katika baadhi ya maeneo hata kabla ya kukamilika kwa awamu zote, ili kupunguza ukali wa tatizo kwa wananchi kwa kuwapa afueni wakati kazi ikiendelea.

Mzee mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alionekana kububujikwa na machozi ya furaha. “Kwa watoto wetu, maji hayataendelea kuwa hadithi ya mateso,” alisema. “Watapata muda wa kusoma badala ya kutumia nusu siku kuchota maji. Na mifugo yetu haitakufa tena kwa kiu.”

Katibu Mkuu, Mhandisi Mwajuma alimtaka mkandarasi kuhakikisha baadhi ya vijiji vinapata maji mapema hata kabla ya mradi mzima kukamilika kwa asilimia mia, akihimiza kuwa maendeleo lazima yaguse maisha ya wananchi kwa vitendo, na sio maneno

Viongozi na wakilishi wa wananchi katika eneo hilo walipongeza kazi ya Serikali kwa kuanza kutekeleza mradi wa kimkakati wenye lengo la kubadilisha maisha ya wananchi. 

Wakisema ukweli unabaki kuwa vijiji 13 ambavyo havijawahi kuwa na maji tangu uhuru sasa vina matumaini mapya, jambo ambalo linagusa maisha ya wananchi na wafanyabiashara katika kazi zao za kila siku.

Wamesema kuwa Serikali imetenda jambo kubwa ambapo baada ya miaka mingi ya kiu, Monduli sasa itapata ukombozi wa maji.

Katika kila kijiji alichotembelea, Mhandisi Mwajuma hakusikiliza tu ripoti na kutoa maelekezo kwa wahandisi wa maji bali pia alikaa na wananchi, akasikiliza hoja zao, na kuhimiza ushirikiano. “Hakuna mradi wa maji utakaoishi kama wananchi hawajauhusika moja kwa moja,” alisisitiza.

Kazi hiyo ya kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi ilihitimishwa kwa kikao cha kazi na Mamlaka ya Maji Karatu (KARUWASA) pamoja na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma katika jukwaa hilo alisisitiza weledi, bidii na uaminifu katika usimamizi wa miradi ya maji, akionya dhidi ya upotevu wa maji ambao huongeza gharama za uendeshaji. 

Alisisitiza kuwa uwajibikaji na ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, Mamlaka za Maji na wananchi ni msingi wa uendelevu wa miradi na huduma ya kudumu na endelevu.

Ziara ya Mhandisi Mwajuma katika Wilaya za Karatu na Monduli imeacha alama kubwa sio tu kama safari ya kikazi, bali kama ishara ya dira ya Serikali katika Sekta ya Maji. 

Imeonesha jinsi kero ya huduma ya maji inavyoshughulikiwa kwa karibu, kwa mipango ya muda mfupi, kati na mrefu. Imeonesha pia kuwa Serikali inapenda kuona miradi inayotoa maji kwa wananchi, si miradi ya makaratasi.

Kwa wananchi wa Karatu na Monduli, hii si simulizi ya takwimu pekee. Ni ukweli wa watoto watakaoamka asubuhi na kwenda shule pasipo kubeba ndoo na madumu ya maji. Ni ukweli halisi wa akina mama watakaopata muda zaidi wa kushughulika na biashara na majukumu ya msingi katika familia zao. Ni uhakika wa mifugo na mashamba yatakayonufaika kwa huduma ya uhakika ya maji.

Jambo la msingi kabisa ni wananchi kulinda vyanzo vya maji na kuviendeleza pamoja na miundombinu ya miradi ya maji. 

Uharibifu wa mazingira au miundombinu ya maji, matokeo yake yatakua mabaya katika uendelevu wa huduma ya maji kwa sasa na baadae.

Ukweli wa Kijiografia ni kuwa Monduli inasifa ya kuwa na ukavu wa kitropiki, ukilinganisha na maeneo mengine. 

Wakazi wake miongoni mwa kazi zinazowaingizia kipato ukiacha utalii, ni mifugo ambayo inahitaji maji ya kutosha kila wakati, iwe mvua au jua na malisho. Kwa maana hiyo ulinzi na utunzaji wa mazingira, vyanzo vya maji na miundombinu ya miradi ya maji ni jukumu la kila mwananchi katika maeneo haya.

Ukweli ambao pia ni mmbaya unahusu janga la mabadiliko ya tabianchi ambayo moja ya visababishi vinavyochochea ni binadamu na kazi zake ambazo athari na matokeo yake ni pamoja na kupotea kwa vyanzo vya maji na kuhatarisha usalama wa chakula kwa kuporomoka uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa wakulima kutokana na hali ya hewa mbaya. Janga hili linazikumba nchi zilizoendela na zile za ulimwengu wa tatu. 

Hivyo, kila mwananchi ni sharti awe mlinzi wa mazingara ili kuwa na uhakika wa huduma ya maji katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news