NA GODFREY NNKO
OFISI ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imesema kuwa, katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 jumla ya sheria 297 zimefanyiwa marekebisho huku miswada 60 ikipitishwa.
Hayo yamesemwa leo Septemba 11, 2025 na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw.Onorius John Njole wakati akiwasilisha mada kuhusu ofisi hiyo katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
Amesema,lengo ni kuhakikisha kila wakati watumiaji wanakuwa na sheria ambazo zimehuishwa ili kukidhi matarajio na kuleta matokeo chanya kiuchumi na kijamii.
Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema kuwa, pia katika kipindi hicho jumla ya sheria zilizofanyiwa urekebu ni 446 ambapo sheria zilizofanyiwa tafsri ni 433.
"Na katika kipindi hicho cha miaka mitano, jumla ya sheria ndogo zilizotengenezwa ni 5,708,miongoni mwa sababu za kufanya hivyo, ni kutokana na mahitaji mahususi ikiwemo mabadiliko ya mazingira."
Amesema, miongoni mwa matarajio ya ofisi hiyo ni kuongezeka kwa ubora na ufanisi katika huduma za uandishi wa habari nchini.
Vilevile,kuimarika kwa taswira na kujenga imani katika mfumo wa sheria ikiwemo kukua kwa uwezo na umahiri wa waandishi wa sheria.
"Matarajio mengine ni kuona ongezeko la ushirikishwaji wadau katika mchakato wa utungaji sheria ili kukidhi matarajio ya umma ya kupata sheria zinazojibu changamoto za jamii, kupata sheria kwa urahisi na kupata sheria fasaha kwa utekelezaji bora," amefafanua Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Ikumbukwe kuwa, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ina jukumu la msingi la kubadili sera kuwa sheria ambazo zinasaidia upatikanaji wa haki,usawa na maendeleo.
Kwa mujibu wa Mwandishi Mkuu wa Sheria,watumishi wa ofisi hiyo ambao ni waandishi wa sheria, mawakili wa serikali, warekebu wa sheria, makatibu sheria na watumishi wengine ni msingi wa kazi zao wakileta utaalamu,uadilifu na kujitolea katika kila jukumu la kutunga sheria.
Tangu ilipoanzishwa kama sehemu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, OCPD imeendelea kutekeleza maono ya dira yake kuwa kitovu cha ubora katika uandishi wa sheria.
"Jukumu letu huanza pale ambapo hitaji la sheria linapotambuliwa na tunaendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uandishi wa sheria, vikao vya Bunge na hata baada ya sheria kupitishwa, tunahakikisha kwamba sheria zilizotungwa zinakidhi kwa ufanisi.
"Huduma zetu zinalenga kutoa sheria bora, zinazopatikana kwa urahisi na kwa usahihi kwa ajili ya kujenga msingi imara kwa maendeleo endelevu.
"Zaidi ya uandishi wa sheria, tunashirikiana kwa karibu na Bunge, Mahakama, taasisi za serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa sheria zinapatikana kwa lugha rahisi ili kukidhi dhamira yetu ya upatikanaji wa sheria bora kwa kila mtu."
OCPD pia imedhamiria kukuza ushirikiano utakaochangia uthabiti wa kiuchumi, ukuaji wa maendeleo na haki za binadamu na kujenga msingi endelevu.
Tags
Habari
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria
