Serikali yawaweka juu Watanzania kupitia maji ya kimataifa

DAR-Jiografia inaonesha kuwa,maji yanaweza kutumika katika zaidi ya nchi moja pamoja na mabara. Ni kusema kuwa,maji hayana mipaka yanapotiririka kutoka eneo moja hadi jingine, hivyo yanawafikia wahitaji wa aina tofauti tofauti na kwa matumizi mbalimbali.
Waziri wa Maji nchini Tanzania, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), wa kwanza kushoto, pamoja na Waziri wa Maji nchini Malawi Mhe. Abida Sidik Mia na Waziri wa Maji nchini Msumbiji, Mhe. Carlos Mesquita wakionesha mkataba waliosaini wa makubaliano na ushirikiano baina ya nchi hizo tatu katika kuweka mikakati ya pamoja katika utunzaji, ulinzi na uendelezaji wa Bonde la Mto Ruvuma, hafla iliyofanyika jijini Dar es salaam, tarehe 31 Julai,2024.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na hazina ya rasilimali nyingi za maji, zikiwemo zile zinazovuka mipaka ya kitaifa na kuhusisha taifa zaidi ya moja. 

Hadi sasa, Tanzania ina jumla ya mabonde saba ya maji ambayo yanahusisha ushirikiano wa majirani kutokana na maji yake kuvuka mipaka ya nchi, maarufu kama majishirikishi au maji ya kimataifa.

Maji haya ni vyanzo vya maji ikihusisha maziwa sita (6) yakiwamo maziwa ya Victoria, Tanganyika, Nyasa, Chala, Jipe na Natron; na mito nane (8) ambayo ni Mara, Kagera, Songwe, Ruvuma, Umba, Malagarasi, Momba na Mwiruzi. 

Usimamizi wa rasilimali hizi ni suala la kimkakati, kisiasa na kijamii, kwani huchangia si tu ustawi wa Tanzania bali pia ustawi wa nchi jirani na watu wake.

Hadi kufika mwezi Aprili 2025, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutekeleza kwa mafanikio makubwa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za majishirikishi kupitia ushirikiano thabiti na nchi jirani na taasisi za kikanda na kimataifa. 

Taasisi hizi ziliundwa mahsusi kuwezesha usimamizi wa pamoja wa vyanzo vya maji vinavyogusa zaidi ya taifa moja, huku miradi mbalimbali ya maendeleo ikiendelea kutekelezwa kwa mafanikio.

Moja ya taasisi hizo ni Kamisheni ya Bonde la Mto Nile ambayo ni mfano hai wa mafanikio ya ushirikiano tajwa. 

Kamisheni hii ilianza kazi rasmi tarehe 13 Oktoba 2024 baada ya nchi sita za Tanzania, Uganda, Ethiopia, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini kukamilisha utekelezaji wa Makubaliano ya Mfumo wa Ushirikiano wa Bonde la Mto Nile (CFA).

Hivi sasa, maandalizi ya uzinduzi rasmi wa Kamisheni hiyo na Wakuu wa Nchi na Serikali yanaendelea na yanatarajiwa kufanyika mwaka 2025. 

Sambamba na hilo, taratibu za kuhamisha shughuli kutoka Taasisi ya Mpito ya Nile Basin Initiative (NBI) kwenda kwenye Kamisheni kamili ya Nile River Basin Commission (NRBC) zinafanyika kwa kasi.

Kupitia Kamisheni hiyo, Tanzania inatekeleza Mradi wa Usimamizi wa Maji Chini ya Ardhi katika Mwambamaji wa Kagera kwa kushirikiana na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda. 

Mradi husika unathamani ya Dola za Marekani 5,329,452/= kupitia ufadhili wa Mfuko wa Mazingira Duniani (Global Environmental Facility-GEF) na hadi Aprili 2025, mradi huo utekelezaji ulikuwa katika hatua za ununuzi wa vifaa vya kupima kiasi na ubora wa maji chini ya ardhi. 

Aidha, mradi wa kuzalisha umeme kupitia Maporomoko ya mto Kagera, eneo la Rusumo umekamilika, na Tanzania inanufaika na umeme kiasi cha megawati 26.7 ambazo tayari zimeunganishwa katika Gridi ya Taifa.

Katika upande mwingine, Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe imeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Tanzania na Malawi kupitia utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Bonde hilo. 

Programu hiyo inalenga kudhibiti mafuriko kwa kufanya ujenzi wa mabwawa yatakayosaidia pia kuzalisha umeme, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, pamoja na matumizi mengine ya kijamii na kiuchumi.

Mapema mwezi Desemba 2024, Tanzania ilishiriki kikamilifu katika makabidhiano ya Ofisi Kuu za Kamisheni ya Bonde la Songwe yaliyofanyika Kyela, mkoani Mbeya. 

Kwa sasa, juhudi zinaelekezwa kwenye utafutaji wa fedha za utekelezaji wa miradi husika ambapo Tanzania na nchi jirani ya Malawi tayari zimewasilisha maombi ya ufadhili kwa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (IFC) na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Katika ukanda wa Ziwa Victoria, kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Serikali ya Tanzania inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya majitaka katika Jiji la Mwanza kupitia Programu ya Pamoja ya Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji ya Bonde hilo. 

Kazi zote hizi matokeo yake ni kunufaisha wakazi na wananchi katika maeneo husika. Mradi huu upo katika hatua ya manunuzi ya mkandarasi. 

Aidha, nyongeza ya fedha kiasi cha Euro 7,860,000 kutoka Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya (EU) imepatikana ili kupanua mtandao wa majitaka na kuongeza uwezo wa taasisi zinazohusika.

Pamoja na hilo, Wizara ya Maji inaratibu maandalizi ya mradi mkubwa wa kisekta Regional Multisectoral Multiphase Programme for Lake Victoria Basin unaotarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani milioni 450 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) kupitia Dirisha la IDA 21. 

Mradi huo unaendana na vipaumbele vya taifa, hasa usimamizi wa rasilimali za maji na mazingira katika Bonde la Victoria.

Kwa upande wa Kusini, Kamisheni ya Bonde la Mto Ruvuma imepiga hatua kubwa ambapo mnamo Julai 2024, nchi za Tanzania, Msumbiji na Malawi zilisaini Hati ya Makubaliano ya Usimamizi wa Pamoja wa Bonde la Mto huo. 

Hati hiyo imeweka msingi wa kuanzishwa kwa Sekretarieti ya Mpito yenye Makao Makuu mkoani Mtwara, na Tanzania itasimamia shughuli zote za Kamisheni hiyo. 

Hivi sasa, Tanzania kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo na nchi wanachama, ipo katika mchakato wa kuandaa Mradi wa Usimamizi wa Mazingira wa Bonde hilo, mradi ambao unatarajiwa kufadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF).

Mbali na miradi hiyo, Serikali kupitia Sekta ya Maji imeandaa maandiko ya miradi mingine mikubwa ya kimkakati. 

Moja ya miradi ni wa kuimarisha chanzo cha bonde hadi ukanda wa pwani kwa usalama wa viumbehai, "Strengthening Integrated Transboundary Source-to-Sea Management of the Ruvuma River Basin and its Coastal Zones to Ensure Ecosystem Health and Livelihood Security" unaotarajiwa kugharimu Dola za Marekani 7,763,000, kwa ushirikiano na nchi za Msumbiji, Malawi, mashirika ya IUCN na Global Water Partnership Southern Africa (GWPSA).

Pamoja na hilo, mradi mwingine ni kubaini maji chini ya ardhi ya mlima Kilimanjaro, "Unlocking the Groundwater Potential of the Kilimanjaro Water Tower" wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 8, utakaotekelezwa kwa kushirikiana na nchi ya Kenya, mashirika ya FAO na UNESCO. 

Aidha, mradi wa Kuimarisha bonde la Zambezi dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, "Strengthening Zambezi River Basin Management Towards Climate Resilience and Ecosystem Health" unaotarajiwa kugharimu Dola za Marekani 10,566,750 utafanyika kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Maandiko ya miradi hii yote yamewasilishwa Sekretarieti ya GEF kwa hatua zaidi za utekelezaji.

Ni wazi kuwa Serikali ya Tanzania inafanya kazi kubwa katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za majishirikishi na sio za kubahatisha.

Haya yanafanyika ili wananchi wapige hatua kiuchumi na maendeleo kwa ujumla. Ni juhudi makini, zenye dira ya kitaifa na mwamko wa kimataifa wa kuhakikisha rasilimali hizi muhimu zinalindwa, zinatumiwa kwa uendelevu na zinawanufaisha wananchi wote si wa Tanzania pekee, bali pia wa nchi jirani.

Kwa maantiki hiyo, Tanzania inajidhihirisha kama kinara wa diplomasia ya maji na mfano bora wa usimamizi jumuishi wa mazingira barani Afrika.

“Hili ni somo kwa Afrika. Maji yanaweza kuwa daraja la mshikamano kuliko chanzo cha migogoro,” anasema Profesa Mark Mwandosya, mtaalamu wa Mazingira na Maji na Waziri wa zamani wa Maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news