TAKUKURU Mwanga yaokoa shilingi milioni 24 za NHIF

KILIMANJARO-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kurejesha kiasi cha shilingi 24,182,020 kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),baada ya kushinda kesi ya jinai namba 25889/2024 dhidi ya Bi.Hadija Athumani Ramadhani ambaye ni mwalimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.
Bi.Ramadhani alikuwa anatuhumiwa kwa makosa matatu ambayo ni Kughushi chini ya vifungu vya 333,335(a) na 337 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu Marejeo ya Mwaka 2002,

Pia,kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo chini ya kifungu cha 342 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Marejeo ya Mwaka 2002 na kuusababishia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hasara ya shilingi 48,364,040 chini ya jedwali namba 10 pamoja na vifungu vya 57 na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi marejeo ya mwaka 2002.

Mtuhumiwa alifanya udanganyifu kwa kutengeneza cheti feki cha ndoa ili kumuongeza mtegemezi ambaye alidai kuwa ni mume wake na kukiwasilisha kwa mwajiri wake na kupelekea mtu huyo aliyemuongeza kama mwenza wake kupata matibabu kinyume na utaratibu.

Wakili wa Serikali, Bi. Furahini Kibanga alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga, Mhe.Baraka Kabururu kuwa, mshtakiwa alikiri makosa yake kupitia makubaliano ya maelewano ya kukiri kosa (Plea Bargain) yaliyofanyika kati yake na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Mnamo Septemba 18, 2025, Mahakama ilimpata Bi.Hadija na hatia baada ya kukiri makosa na kutia saini mkataba wa makubaliano.

Mahakama ilimhukumu kurejesha kiasi cha shilingi 24,182,020 na kumhukumu kifungo cha nje cha miezi mitatu.

Aidha,tayari kiasi cha shilingi 12,091,010 kimesharejeshwa NHIF na kiasi kilichosalia kitaendelea kulipwa kwa awamu.

TAKUKURU Wilaya ya Mwanga imesisitiza kuwa,itaendelea kusimamia uwajibikaji wa matumizi ya rasilimali za umma na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu na rushwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news