TBS kuanzisha viwango vipya vya ufanisi wa nishati kwa vifaa vya umeme majumbani

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS),washirika wa maendeleo na Wizara ya Nishati wameanza kuandaa viwango vya ufanisi wa nishati kwa vifaa vya umeme wa majumbani nchini.
"Serikali inalenga kuboresha upatikanaji wa nishati safi,kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kutunza mazingira huku ikiokoa maisha kupitia suluhisho endelevu la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

"Kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS),washirika wa maendeleo na Wizara ya Nishati, Serikali imeanza kuandaa viwango vya ufanisi wa nishati kwa vifaa vya umeme wa majumbani nchini;

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi ameyasema hayo leo Septemba 18,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Dkt.Katunzi ameongeza kuwa, pia vifaa vya maabara vya kisasa vinaendelea kununuliwa kwa ajili ya kuhakikisha vifaa vinavyoingia sokoni vinakidhi viwango vilivyowekwa kabla ya kuwafikia watumiaji.
"Hatua hii inalenga kupunguza uzalishaji wa gesi joto, kupunguza upotevu wa nishati, na hivyo kupunguza gharama kwa watumiaji."

Mbali na hayo, Dkt.Katunzi amefafanua kuwa,shirika hilo linaendelea kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma zake mbalimbali kama vile leseni ya ubora.

Pia,ukaguzi wa shehena zinazotoka nje ya nchi na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi, majengo, maeneo ya uzalishaji, uuzaji, vyombo vya usambazaji wa bidhaa za chakula na vipodozi.

"Mifumo hiyo ni OAS na i-SQMT. Aidha,shirika limeboresha huduma zake kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini kwa kuunganisha mfumo wake unaoitwa Online Application System na mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Tanzania electronic Single Window System TeSWS)."
Dkt. Katunzi amesema, mfanyabiashara anatuma maombi na anapata huduma za taasisi zote na kibali kupitia mfumo huo.

TBS ambayo ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma yanayosimamiwa ba Ofisi ya Msajili wa Hazina huku likiwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara,lilianzishwa kama sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya sekta za viwanda na biashara.

Lengo ni kukuza uchumi wa Taifa na linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Viwango Sura 130.
Katika hatua nyingine, Dkt.Katunzi amesema, Serikali kupitia TBS imetumia zaidi ya shilingi bilioni 9.8 kwa ajili ya kuimarisha ofisi tisa za kanda ikiwemo Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam na Dodoma.

Nyingine ni Kigoma, Mbeya, Pwani na Geita pamoja na ofisi za mipakani ikiwemo Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea, Namanga, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Pia, amesema kuna Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Sirari, Kabanga, Rusumo, Mutukula, Kasesya, Bandari ya Bagamoyo,Bandari ya Mbweni,Bandari ya Dar es Salaam,Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere Dar es Salaam na Bandari ya Tanga.
"Na kwa kuongeza ofisi mpya za kanda, wafanyakazi na vitendea kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakati na kuimarisha zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara katika soko ili kupunguza bidhaa hafifu sokoni na hatimaye kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama,"amesisitiza Dkt.Katunzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news