DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imechangia mashine ya kudurufu nakala (photocopy Machine)katika shule ya sekondari Ubungo NHC, mashine hiyo itasaidia na kurahisisha huduma za kutoa na kuchapisha nakala mbalimbali hususani mitihani ya wanafunzi. 

Makabidhiano hayo yalifanyika katika shule ya Sekondari Ubungo NHC jijini Dar es Salaam, tarehe 24 Septemba,2025.
Kaimu Meneja Masoko na Uhusiano, Bi.Monica Mutoni alikabidhi mashine hiyo kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladslaus Chang’a.
"Tulipokea maombi yenu na kuyafanyia kazi, hivyo tunaamini kuwa, uwepo wa mashine hii utaongeza motisha na fursa kwa walimu kuandaa majaribio na mitihani ya mara kwa mara ili kupima uwezo wa wanafunzi na kuleta matokeo chanya ya ufaulu.
"Tunatamani kuona viwango vya ufaulu vinaongezeka hapa Ubungo NHC na kwa shule za Serikali zote kwa ujumla,"amesema Bi.Monica.
Aidha, Bi. Monica alisema, kupitia mashine hiyo, shule itasaidia kupunguza gharama kubwa ya uendeshaji hasa kipindi cha mitihani.

Vilevile, aliwakumbusha walimu kutumia fursa za mafunzo ya vitendo kwa kuwapeleka wanafunzi katika ofisi za TMA zilizopo Ubungo Plaza na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ili waweze kujifunza masuala ya sayansi ya hali ya hewa.
Awali, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Mkuu wa Shule, Bi.Dorice Kanyabuhula, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ubungo NHC, aliishukuru TMA kwa kutekeleza ombi lao la mashine na alisisitiza kupitia msaada huo, shule itaweza kuandaa mitihani kwa usiri na kupunguza usumbufu wa kuchapisha mitihani nje ya shule.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Shule ya Sekondari Ubungo NHC
Tanzania Meteorological Agency (TMA)

