Wahariri wakumbushwa wajibu wa kitaaluma katika kuripoti masuala ya Sheria kwa weledi na uadilifu

NA GODFREY NNKO
Dodoma

NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.Samwel Maneno amesema kuwa, ofisi hiyo inatambua nguvu kubwa ya vyombo vya habari katika kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi kuhusu haki na wajibu wa kila Mtanzania kupitia mifumo sahihi iliyowekwa na Serikali.
Ameyasema hayo leo Septemba 11,2025 wakati akifungua kikao kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni zao la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo majukumu yake yanaelezwa katika Ibara ya 59(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.

Sambamba na Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa mwaka 2018 pamoja na Tangazo la Serikali Namba 48 la mwaka 2018.

Pamoja na majukumu mengine, ofisi hiyo inawajibika kutoa ushauri kwa wizara, idara za Serikali na taasisi nyingine za Serikali na mashirika ya umma kuhusu mchakato wa kutunga sheria na ushauri wa kisheria katika masuala ya jumla na katika uandaaji wa miswada kwa ajili ya kupitishwa na Bunge ili kuwa sheria.

"Kwa hiyo, hii ni fursa muhimu sana kwenu,"ameeleza Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku akisema kuwa,wahariri watapata uelewa mpana kuhusu namna ya kuripoti habari zinazohusu masuala ya kisheria kwa weledi ili kuwapa wananchi fursa ya kuzifahamu katika kujiletea maendeleo.

Amesema, kupitia Ofisi ya Mwanasdheria Mkuu wa Serikali ambayo ni chanzo sahihi chenye wajibu wa kikatiba katika masuala ya sheria ni fursa muhimu ambapo wakiitumia vizuri wana nafasi nzuri ya kuripoti taarifa sahihi zenye maudhui yaliyopo na namna ambavyo masuala ya kisheria yanashughulikiwa na Serikali.

Katika hatua nyingine, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa, katika mwaka uliopita ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemio kufanikiwa kuandaa miswaada 19 ya kisheria, pia imetafsri sheria 433 kati ya sheria 446 zilizopo hapa nchini kutoka kwenye lugha ya Kiingereza kwenda kwenye lugha ya Kiswahili.

Amesema, lengo la kufanya hivyo, ni ili kuwapa wananchi uwanda mpana wa kuzisoma sheria hizo na kuzielewa ili kutambua umuhimu wa utii wa sheria bila shuruti.

Kupitia tafsri hizo ambapo kwa sasa zimesalia 13 kukamilisha utafsri huo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema, utaendelea kuwajengea wananchi uwezo zaidi wa kuzifahamu sheria hizo.

Pia,amesema wamefanikisha maazimio mawili katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na urekebu wa sheria 446 nchini, ambapo kwa sasa zimeshazinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Msheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan na zinafanya kazi.

Aidha, ofisi hiyo imefanikisha upekuzi wa mikataba 3,446 ya kitaifa na kimataifa ambayo inahusisha ununuzi, ujenzi, ukarabati na utoaji huduma kwa jamii,

Pia, zaidi ya makubaliano ya awali (MoU) 700 yalifanyiwa ukaguzi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuyapitia na kutoa ushauri kwa ajili ya hatua zingine.

Awali Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi.Leila Mhanji amesema kuwa, lengo la kikao kazi hiki ni kuwafahamisha majukumu yanayotekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kujenga mahusiano ya karibu baina ya ofisi hiyo na wahariri.

Msemaji Mkuu wa Serikali

Akizungumza kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali,Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw.Rodney Mbuya ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa kikao kazi hiki muhimu ambacho kimewaleta pamoja wahariri ili waweze kujifunza mengi kuhusu ofisi hiyo.

"Hii ni fursa pekee ambayo mmeipata kwa ajili ya kuifahamu ofisi hii vizuri ili kuzifahamu sheria, hivyo endeleeni kuonesha ushirikiano.Tuendelee kusimamia misingi na weledi wa uandishi wa habari ili kuhakikisha nchi yetu tunaipeleka katika njia nyoofu na hasa katika maendeleo."

Aidha, ameendelea kuwahimiza kutumia vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali kwa kuzingatia maadili,sheria na weledi ili kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi na kamilifu hususani kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu.

Vilevile, amewataka wanahabari nchini kuendelea kufuata sheria za nchi ili taaluma ya habari iendelee kuwa na hadhi kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news