Waliomaliza vifungo magerezani wafundwa

NA DIRAMAKINI

Wafungwa waliomaliza vifungo vyao magerezani wameshauriwa kuepuka vitendo ambayo vitakavyowafanya warudie kifungoni badala yake wajikite katika maswala ya kimaendeleo kwa manufaa yao ya kimaisha.
Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa taasisi ya kuhudumia wafungwa waliomaliza muda wao wa vifungo magarezani ya Tanzania Ex-Prisoners Foundation (TEPF) Rose Malle, wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na cheti cha pongezi ilichopata taasisi hiyo hivi karibuni, kutokana na shughuli inazofanya.

“Adhabu ya kifungo ni sehemu ya maisha ambayo si vyema mtu akairudia, badala yake mtu anapopata fursa ya kutoka kifungoni aidha kwa kumaliza muda wake wa kifungo au kwa sababu nyingine yoyote hana budi kujikita katika shughuli za maendeleo huku akizingatia maadili mema."

Akizungumzia cheti hicho, Malle alisema kuwa kilitolewa na Idara ya Magereza nchini katika kutambua mchango wa taasisi hiyo katika kuwasaidia wafungwa waliomaliza muda wao magerezani ili warudi kwenye maisha ya zamani yenye maadili mema.

“Tulikabidhiwa cheti hiki na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Agosti 26, mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 tangu kuanzishwa kwa taasisi ya Magereza hapa nchini.

“Tuzo hii imetutia moyo sana; imetupa ari ya kufanya vizuri zaidi kwa vile sasa tuna uhakika shughuli zetu zinatambulikana na kuthaminiwa na serikali kupitia Idara yake ya Magereza hapa nchini.”

Akizungumzia shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo, Malle alisema ni pamoja kuwapa elimu wafungwa waliomaliza muda wao ili waweze kufanya shughuli zitakazowawezesha kujikimu na kuendelea na maisha baada ya adhabu walizotumikia.

“Elimu hizo ni pamoja na ya ujasiriamali, sambamba na ile ya ufundi; elimu wanazopata zitawawezesha kupata ajira au kujiajiri wenyewe na hivyo kuweza kujikimu kimaisha wao na wanafamilia wao kwa wale wenye familia."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news