GEITA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Majaliwa amepokelewa na Meneja wa Idara ya Mawasiliano wa Benki Kuu, Bi. Victoria Msina ambapo amepewa maelezo kuhusu Mpango wa Benki Kuu wa Ununuzi wa Dhahabu ulioanza Oktoba 1,2024.
Mpango huo umeleta mafanikio makubwa katika kuongeza hifadhi ya fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Hadi kufikia Agosti 2025, jumla ya tani 9.165 za dhahabu zenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 1,015.98 zimeshanunuliwa.
Vilevile, mpango huo umefungua fursa kwa wachimbaji na wauzaji wa dhahabu nchini kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu ya Tanzania kwa bei ya ushindani kulingana na soko la kimataifa.
Aidha,Benki Kuu imepewa tuzo maalum kwa udhamini wa ujenzi ya miundombinu ya kudumu katika viwanja vya Maonesho hayo yanayofanyika kuanzia Septemba 18 hadi 28, 2025.




