MANYARA-Mahakama ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara imemtia hatiani Afisa Msitu wa Suledo wilayani humo,Bw.Siloma Manyindo Mtero kwa makosa ya rushwa.
Hukumu hiyo ya shauri la jinai Na.03/2025 kati ya Jamhuri dhidi ya Afisa huyo imetolewa Oktoba 10,2025 na Hakimu Mkazi,Mheshimiwa Boniface Lihamwike
Katika kesi hiyo, mshtakiwa ametiwa hatiani kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) na 15(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 marejeo ya 2023.
Mshtakiwa alitenda makosa hayo kwa kuomba kiasi cha shilingi 600,000 kwa wakulima wa Kata ya Sunya na kuwapa ahadi ya kuwasogezea mipaka ya Msitu wa Suledo.
Lengo ni ili waweze kufanya shughuli za kilimo katika hifadhi hiyo ya msitu, kitendo ambacho ni kinyume na sheria na kanuni za Hifadhi ya Msitu wa Suledo.
Kesi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Bw.Abdulrahim Jamal Mockray.
Mahakama imemtia hatiani na kuamuru kulipia faini ya kiasi cha shilingi 500,000 kwa kila kosa au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela endapo atashindwa kulipa faini hiyo.Aidha,mtuhumiwa alilipa faini ya shilingi 1,000,000.
Tags
Habari
Hifadhi ya Msitu wa Suledo
Mahakamani Leo
Maliasili na Utalii
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
