Agizo la Rais Dkt.Samia uchimbaji wa visima vya umwagiliaji Geita latekelezwa

GEITA-Siku chache baada ya Maelekezo ya Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Geita kuelekeza visima 20 vya umwagiliaji vichimbwe mkoani humo,na Waziri wa Kilimo,Husein Bashe kuitaka NIRC kutekeleza agizo hilo,utekelezaji umeanza.
Zaidi ya wananchi 747 wanatarajiwa kunufaika na mradi wa uchimbaji visima vya Umwagiliaji 36 unaotekelezwa katika Kijiji cha Mwilima mkoani Geita, ambapo visima hivyo vitamwagilia zaidi ya ekari 1,440 katika vijiji 32, lengo ikiwa ni kuongeza uzalishaji wa mazao na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uchimbaji wa visima hivyo,Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe.Martin Shigela amesema kuwa,utekelzaji wa mradi huo utachangia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza ajira, kuongeza thamani ya mazao na kurahisisha upatikanaji wa chakula na mazao ya biashara kwa wananchi wa Kijiji cha Mwilima.
Aidha, Mhe. Shigela ametumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha usalama wa vifaa na mitambo ya umwagiliaji,unakuwa wa kutosha kwakila mmoja kushiriki katika ulinzi wa rasilimali hizo ili kuhakikisha mradi unadumu kwa muda mrefu.

Aidha,  Mhandisi Umwagiliaji Mkoa wa Geita Boniface Mkita amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali kupitia Tume inaendelea na utekelezaji wa kazi ya uchimbaji wa visima kwa kutumia mitambo ya Serikali.

Pia ameongeza kuwa kwa awamu ya kwanza, visima 36 vitachimbwa katika vijiji 32 Mkoani humo, ambapo ekari 1,440 zitamwagiliwa na kuhudumia wakulima zaidi ya 747.

Utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa ushirikiano kati ya Tume na halmashauri husika, na unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili (2). Kati ya visima hivyo, visima 30 tayari vimefanyiwa uhakiki wa awali.

Mhandisi Mkita amesema kuwa kilimo cha Umwagiliaji kitawawezesha wakulima kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya uzalishaji wa mazao, pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao yenye thamani kubwa yatakayowapatia wakulima kipato kikubwa kutoka eneo dogo.
Miongoni mwa kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na utafiti na upimaji wa maeneo ya uchimbaji, uchimbaji wa visima vyenye urefu usiozidi mita 250, uwekaji wa mabomba yenye kipenyo cha inchi 6 hadi 8, pamoja na ufungaji wa mifumo ya kusukuma maji kwa kutumia pampu.

Sambamba na hayo ,kutajengwa minara ya kuwekea tenki za maji, kununuliwa na kufungwa matanki yenye ujazo wa lita 10,000, pamoja na mabomba ya inchi 3 yatakayofikisha maji shambani.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mwilima akiwemo Ndagaile Lusanda na Stephano Malehe wameishukuru serikali kwani visima hivyo vitasaidia kuinua vipato vyao kwa kulima mazao ya mbogamboga pamoja na mazao mengine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news