NA LWAGA MWAMBANDE
RAILA Amolo Odinga maarufu kama Baba ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kenya na kiongozi mahiri kupitia kambi ya upinzani nchini humo amefariki dunia leo Oktoba 15,2025 akiwa na umri wa miaka 80.
Taarifa za awali zilidokeza kuwa, Raila Odinga amekumbwa na shambulio la moyo alipokuwa akitembea asubuhi akifanya mazoezi jimboni Kerala lililopo Kochi nchini India, alikuwa akiendelea na matibabu ndipo akakimbizwa Hospitali ya Devamatha ambapo alithibitishwa kufariki dunia.
Kwa sasa, Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt.William Ruto ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa na kusema kuwa,mwili wa Odinga utarejeshwa Kenya kwa mazishi ya kitaifa. Bendera zitapepea nusu mlingoti kote nchini na katika balozi za Kenya nje ya nchi.
Raila Odinga alijulikana kwa juhudi zake za kuleta mabadiliko nchini Kenya. Alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliopigania mfumo wa vyama vingi na kuanzishwa kwa Katiba mpya ya mwaka 2010.
Pia alihusika katika kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi wa 2007. Ingawa alikumbwa na changamoto nyingi kisiasa, alibaki kuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa na alihusishwa na harakati za demokrasia na haki za binadamu.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, kifo cha Raila Amolo Odinga kimeacha pengo kubwa katika siasa za Kenya na Afrika Mashariki na atakumbukwa kama kiongozi aliyejitolea kwa ajili ya haki, demokrasia na ustawi wa wananchi. Endelea;
1. Tulikuwa nao watu, miamba ya enzi zao,
Jinsi walifanya vitu, na mitikisiko yao,
Ila sasa si wenzetu, wamekwishakwenda zao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
2. Raila huyu ni mtu, sio wa nyumbani kwao,
Kote kuliko na utu, naye kulikuwa kwao,
Amefanya vingi vitu, heri kuliko mafao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
3. Kwa siasa kule Kenya, alikuwa ni wa kwao,
Na sisi nje ya Kenya, tulisikiliza wao,
Mambo mengi alifanya, ni mema kwetu na kwao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
4. Kweli ni mtu mzima, umri likuwa nao,
Ila Wakenya kwa wema, walifanya mambo yao,
Wakampa jina jema, kumuita baba yao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
5. Yeye aliitwa baba, sababu wanazo wao,
Mambo yake siyo haba, mazuri kwetu na kwao,
Kwa siasa alishiba, huyo kiongozi wao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
6. Hii demokrasia, kama ilianza kwao,
Baba yake kuanzia, na Baba Kenyatta hao,
Mengi walipigania, licha tofauti zao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
7. Toka ujana Raila, Kenya huyo mtu wao,
Kisiasa hakulala, kila siku yuko nao,
Hata alifungwa jela, mambo ya siasa zao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
8. Siasa za vyama vingi, Kenya walifanya yao,
Kura jambo la msingi, kwa zile sauti zao,
Ngeweza ingia kingi, kama si vurugu zao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
9. Elfu mbili na saba, ule uchaguzi wao,
Kura hakupata haba, kwa zile hesabu zao,
Njia zote waliziba, juu wabakie wao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
10. Vurugu lipotokea, chinjana wao kwa wao,
Amani ilitokea, kwa wanasiasa hao,
Meza kuisogelea, kuyamaliza ya kwao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
11. Kama si hekima yao, yaliyotokea kwao,
Ngezidi chinjana hao, nchi isiwe ya kwao,
Utu alikuwa nao, zikaisha shida zao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
12. Raila kwenye siasa, ukuu wake anao,
Ile ya kwake hamasa, alivuta watu hao,
Nguvu hatunayo sasa, kwa wengine kazi kwao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye
13. Pole kwa nchi ya Kenya, kufa kiongozi wao,
Familia huko Kenya, ndugu na jamaa hao,
Na hata nje ya Kenya, mwanamajumui wao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
14. Huu ukurasa mpya, siasa za huko kwao,
Nani atapiga chafya, asikilizwe na wao,
Tunachotaka ni afya, amani nchini mwao,
Baba Raila Odinga, naye sasa hatunaye.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
