NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imetangaza msamaha wa kipekee kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya watakaojitokeza wenyewe na kuomba msamaha kwa Watanzania, wakiahidi kuachana kabisa na biashara hiyo haramu.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 3,2025 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kiwanda cha Twiga kilichopo Wazo jijini Dar es Salaam katika zoezi la kuteketeza zaidi ya tani 4.4 za dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, mamlaka iko tayari kuwasamehe kwa hiari watu wote waliowahi kujihusisha na wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, endapo watatubu kwa dhati, kujisalimisha kwa DCEA, na kuwaomba Watanzania radhi.
"Tunachowaomba waje, wawaombe radhi Watanzania ambao wamewaharibu kwa biashara yao ya dawa za kulevya na kuwahakikishia kwamba hawataendelea tena na biashara hiyo.Wakifanya hivyo, tutawasamehe na hatutawachukulia hatua za kisheria,"amesema Kamishna Jenerali Lyimo.Kamishna Jenerali Lyimo amefichua kuwa, DCEA inaendesha operesheni kabambe inayolenga kuwakamata wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.
Amesisitiza kuwa,hakuna atakayesalimika na kwamba juhudi za kuwakamata wale waliotorokea nje ya nchi na wengine kuingia mafichoni zinaendelea kwa karibu.
"Nchi walizokimbilia tunazifahamu, na tunaendelea kuwafuatilia huko huko. Tunawahimiza wajitokeze, waombe msamaha, na waahidi kutorudia tena biashara hii haramu,wanaweza kufika wenyewe mamlaka au kupiga simu bure kupitia namba 119 ," ameongeza.
Kamishna huyo amesema kuwa, tayari wafanyabiashara wengi wakubwa maarufu kama mapapa wamekamatwa na kuhukumiwa, baadhi yao wakipewa adhabu ya kifungo cha maisha jela au miaka 30. Aliwataka waliobaki kuacha mara moja, kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria.
"Dawa za kulevya ni chanzo cha vurugu, ukosefu wa amani na uharibifu wa miundombinu ya taifa. Serikali haitakubali kuona nchi yetu ikivurugwa na wafanyabiashara wa dawa hizi hatari,"amesema Kamishna Jenerali Lyimo kwa msisitizo.
DCEA imesisitiza kuwa, itaendelea kuimarisha ushirikiano na wananchi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa umma na kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kiutendaji.
"Watumiaji wa dawa za kulevya wamekuwa wakiharibu mali na miundombinu ya umma. Hili haliwezi kuvumilika. Tunawataka Watanzania kushirikiana nasi katika vita hii kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha biashara hii haramu,"ameongeza Kamishna Jenerali Lyimo.
Katika zoezi hilo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza jumla ya kilogramu 4,402.02 za dawa za kulevya kiwandani hapo.
Dawa zilizoteketezwa ni pamoja na kilogramu 2,168.18 za methamphetamine, kilogramu 1,064.29 za heroin, gramu 326.95 za cocaine, kilogramu 515.48 za bangi na kilogramu 653.74 za mirungi.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema, dawa hizo zilihifadhiwa kama vielelezo vya mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani, ambapo baadhi ya mashauri bado yanaendelea kusikilizwa huku mengine yakiwa tayari yametolewa hukumu.
Kwa mashauri ambayo bado hayajakamilika, Kamishna Jenerali Lyimo amesema,Mahakama iliagiza dawa hizo kuteketezwa kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo, kama Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015 inavyotaka vielelezo vya dawa za kulevya kuharibiwa wakati shauri likiendelea au baada ya hukumu kutolewa.
Miongoni mwa mashauri yanayohusiana na dawa zilizoteketezwa ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed iliyohusisha heroin kilogramu 882.71 na methamphetamine kilogramu 2,167.29.
Aidha, mashauri yaliyotolewa hukumu ni pamoja na ya Hassan Azizi aliyepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha, Salum Shaaban Mpangula aliyehukumiwa kifungo cha maisha, Hemed Juma Mrisho maarufu kwa jina la “Hororo” aliyehukumiwa kifungo cha maisha,
Tags
Breaking News
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)





