ZANZIBAR-Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi amechaguliwa tena kuwa Rais wa Zanzibar kufuatia ushindi kishindo aliyoupata katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29,2025.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ( ZEC), Jaji George Joseph Kazi ametangaza matokeo hayo Oktoba 30,2025 katika Ukumbi wa Jaji Mkuu Mstaafu Abdi Mahmoud, Afisi ya Tume ya Uchaguzi, Kilimani, Mkoa wa Mjini Magharibi.Akitangaza matokeo hayo, Jaji George Kazi amesema, Mgombea huyo wa Chama cha Mapinduzi ameshinda kwa kupata kura. 448,832 sawa na asimilia 74.8 ya kura zote halali.
Shangwe, nderemo, vifijo na nyimbo za hamasa kutoka kwa viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi vimesikika ndani ya ukumbi baada ya kuyapokea matokeo hayo ya ushindi yanayomrejesha tena madarakani Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuiongoza Zanzibar kwa Awamu ya Pili.
Dkt. Hussein Ali Mwinyi aliyewania kiti hicho kwa Awamu ya Pili amewashinda wagombea wengine 10 wa Vyama Vya Upinzani waliojitokeza kugombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji George Kazi amemkabidhi Dkt. Mwinyi Cheti Maalum cha Ushindi wa Urais wa Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza baada ya ushindi huo,Rais Mteule Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kazi nzuri ya kusimamia uchaguzi huo pamoja na kuwapongeza wagombea wa kiti cha Rais kwa kuonesha uzalendo na kuwaomba kuweka mbele uzalendo na maslahi ya Taifa.
Pia,Dkt. Mwinyi amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuamua kwa mujibu wa katiba kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

















