Dkt.Mpango amwakilisha Rais Samia katika Mkutano wa Dharura wa Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama ya SADC

MANYARA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameshiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ Troika Summit) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwa njia ya mtandao akiwa Babati mkoani Manyara.
Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Prof. Arthur Peter Mutharika na kuhudhuriwa na wajumbe wa Asasi hiyo Tanzania ambaye ni Mwenyekiti aliyemaliza muda wake na Ufalme wa Eswatini ambaye ni Mwenyekiti ajaye.
Mkutano huo umejadili hali ya kisiasa na usalama katika Jamhuri ya Madagascar kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika hivi karibuni.

Pia umeweka dhamira ya kuunga mkono juhudi za kurejesha hali ya amani na utulivu katika Jamhuri ya Madagascar na kutoa wito kwa wananchi wa Madagascar kuhakikisha njia ya mazungumzo inatumika katika kukabiliana na hali iliyopo hivi sasa na kuachana na vurugu, uporaji na uharibifu wa mali.
Mkutano huo, umeiagiza Sekretarieti ya SADC kuhakikisha inashirikisha wadau muhimu kama vile Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Nchi za Bahari ya Hindi ili kuwa na uratibu wa pamoja katika kutafuta suluhu ya mgogoro nchini Madagascar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news