WASHINGTON-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Viwanda na Biashara ya China (Industrial and Commercial Bank of China-ICBC), Bw. Peter Poon pamoja na Mkurugenzi wa Muundo wa Masoko ya Kimataifa,Bi. Yoyo Ye jijini Washington D.C., Marekani.
Mazungumzo hayo yamefanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia inayoendelea kufanyika kuanzia tarehe 13 hadi 18 Oktoba, 2025 jijini Washington D.C.
Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili namna ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya BoT na ICBC, hususan katika eneo la uhifadhi wa akiba ya nchi. Mazungumzo yamejikita katika fursa za kuongeza uwekezaji kupitia ununuzi na uhifadhi wa dhahabu, hatua itakayosaidia kuongeza akiba ya fedha za kigeni nchini Tanzania.

