Gavana Tutuba aiwakilisha Serikali hafla ya kumuaga Rais wa Tatu wa Afreximbank

CAIRO-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, ameiwakilisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla ya kumuaga Rais wa tatu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ya Uuzaji na Uagizaji Nje ya Afrika (Afreximbank), Prof. Benedict Oramah, na kumkaribisha Rais mpya, Dkt. George Elombi.
Dkt. Elombi anakuwa Rais wa Nne wa Afreximbank akiwa amehudumu katika taasisi hiyo tangu mwaka 1996. Dkt. Elombi ambaye aliapishwa tarehe 25 Oktoba 2025 alimpongeza mtangulizi wake Prof. Oramah na ameahidi kudumisha mafanikio ya Afreximbank katika kustawisha sekta ya fedha barani Afrika na uchumi kiujumla.

Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 24 na 25 Oktoba 2025 jijini Cairo, Misri, iliwakutanisha viongozi wa sekta ya fedha, wakuu wa mabenki, wawakilishi wa serikali, na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya bara la Afrika,.
Viongozi hao walimpongeza Prof. Oramah kwa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi wanachama wa Afrika kupitia programu na mikakati ya ubunifu iliyotekelezwa na benki hiyo pamoja na juhudi za kukuza biashara ya ndani ya bara la Afrika na kupunguza utegemezi wa masoko ya nje.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Oramah alitoa shukrani kwa viongozi mbalimbali wa bara la Afrika kwa ushirikiano wao na kusisitiza umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu, ubunifu wa kiteknolojia, na utafiti wa kiuchumi ili kujenga Afrika yenye kujitegemea kifedha.
Aidha, kupitia Afreximbank, Tanzania inategemea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo kujenga kituo cha umahiri cha afya hapa nchini (African Medical Centre of Excellence).

Afreximbank yenye nchi zaidi ya 50 wanachama, ilianzishwa mwaka 1993 kwa lengo la kukuza biashara ya ndani na nje ya Afrika.

Kupitia miradi kama Intra-African Trade Initiative, Project Preparation Facility, na Pan-African Payment and Settlement System (PAPSS), benki hii imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya viwanda, miundombin na biashara barani Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news