WASHINGTON D.C-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, anashiriki Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia inayofanyika Washington D.C, Marekani kuanzia tarehe 13 hadi 18 Oktoba 2025, yenye kaulimbiu “Misingi ya Ukuaji na Ajira.”
Sambamba na mikutano hiyo, Gavana Tutuba atakuwa na majadiliano na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Bw.Adran Ubisse na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa IMF,Bw. Abebe Selassie.Mikutano hii hufanyika kila mwaka na hukutanisha magavana wa benki kuu, mawaziri wa fedha na maendeleo, wakuu wa sekta binafsi, wawakilishi wa asasi za kiraia, pamoja na wasomi, kwa ajili ya kujadili hali ya uchumi wa dunia na masuala ya kimataifa yenye umuhimu, kama vile mwelekeo wa ukuaji wa uchumi, uthabiti wa kifedha, na kupunguza umaskini.



