Mradi wa maji Mugango-Kiabakari-Butiama na ndoto ya Mwalimu Nyerere

MARA-Kila Oktoba 14, nchi ya Tanzania husimama kwa pamoja kumkumbuka na kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza na Baba wa Taifa hili la Tanzania. Ni sehemu ya utamaduni wa jamii yetu kuwakumbuka wote waliotangulia.
Taswira ya chanzo cha uhakika cha maji kwa mradi wa maji wa Mugango-Kiabakari-Butiama ambalo ni Ziwa Victoria.

Kwa Watanzania siku hii ni siku ya mshikamano na tafakari ya misingi aliyoiacha na alama kubwa kumuenzi Baba wa Taifa letu ikiwemo Umoja, Usawa na Utu.

Mwaka 2025, wakati Taifa likiadhimisha Siku ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wananchi na wakazi wa wa Butiama, Mugango na Kiabakari wanazo sababu za msingi na kipekee za kusherehekea siku hii adhimu.

Hii inachagizwa zaidi na mradi mkubwa wa maji wa Mugango–Kiabakari–Butiama uliotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi za Tanzania Bilioni 70.5, ambapo sasa wananchi wa maeneo hayo wanafurahia huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza, ikiwa ni ishara hai ya ndoto na misingi ambayo Mwalimu aliisimamia enzi za uhai wake.

Mwalimu aliwahi kusisitiza kuwa uhuru haukuwa kubadilisha bendera pekee, bali kuhakikisha Watanzania wanapata uhuru wa kweli jumuishi unaohusisha huduma muhimu za kijamii na kiuchumi. 

Kauli yake maarufu ya, “Uhuru ni Maendeleo,” ilikuwa ni mwongozo wa kipaumbele cha elimu, afya na huduma za kijamii ikiwemo huduma ya majisafi.

Hata hivyo, imechukua muda maeneo ya Mkoa wa Mara, ikiwemo Butiama, kijiji alichozaliwa Mwalimu Julius K. Nyerere yalikuwa na uhaba wa huduma ya maji. Huduma haikutosheleza kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na shughuli mbalimbali za kijamii.

Akina mama na watoto walilazimika kutembea nje ya makazi kutafuta huduma hiyo kwenye vyanzo mbalimbali, vingine vikiwa visivyo salama. Hii ilipoteza muda mwingi kwa kuacha kazi nyingine wakati wa utafutaji wa huduma ya maji.

Mradi wa Mugango–Kiabakari–Butiama sasa umebadilisha kabisa hali hiyo. Ukitegemea maji ya uhakika ya Ziwa Viktoria, ujenzi wa mradi huu umehusisha mitambo ya kisasa ya kusafisha maji, matenki makubwa ya kuhifadhi na mtandao mpana wa mabomba ya usambazaji maji.

Hadi sasa unawanufaisha zaidi ya wakazi laki moja katika vijiji zaidi ya 39 vya Halmashauri za Butiama,Musoma na Bunda. Ni hatua kubwa inayothibitisha mtazamo wa Mwalimu Nyerere kwamba maendeleo lazima yaguse maisha ya mwananchi wa kawaida moja kwa moja.

Kipekee zaidi, mradi huu unahudumia Butiama, ambapo ni makazi ya Baba wa Taifa. Hapa ndipo alipozaliwa miaka 103 iliyopita, ndipo aliporejea kupumzika baada ya majukumu ya kitaifa, na ndipo alipozikwa mwaka 1999. 

Leo, Butiama si tu makumbusho ya historia kupitia Kituo cha Mwalimu Nyerere, bali pia mfano wa dhahiri wa maendeleo yanayoendeleza misingi yake ya kijamii. 

Kupatikana kwa majisafi nyumbani, na maeneo ya umma ikiwemo shuleni, vituo vya magari na vituo vya afya ni ishara ya ndoto zake zilizotimia.

Athari chanya za mradi huu zinaonekana kila mahali. Maeneo ya huko Kiabakari, akina mama waliokuwa wakiamka alfajiri kutembea kilomita kadhaa nje ya makazi yao sasa wanapata huduma ya majisafi karibu. 

“Nilikuwa natembea kilomita sita kila siku kubeba ndoo ya maji. Leo nachota hatua chache kutoka nyumbani,” anasema Mama Maria, mama wa watoto watano. Katika Kituo cha Afya Butiama, huduma zimeimarika kwa kuwa na maji ya uhakika. 

“Huwezi kuendesha hospitali bila maji. Mradi huu umetupa uhai tunaouhitaji,” anasema Dkt. Nangi Nangi-Mganga wa Kituo cha Afya Butiama ambapo utunzaji wa vifaa vya kisasa vya tiba umekuwa bora zaidi.

Kwa wanafunzi, hasa wasichana, mzigo wa kutafuta maji umepungua, hivyo wana muda zaidi wa kushiriki katika masomo na kuwa na utulivu zaidi shuleni. Hili linaakisi imani ya Mwalimu Nyerere kwamba elimu lazima iende sambamba na huduma za kijamii.

Mradi huu wa Mugango ni sehemu ya juhudi pana chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya majisafi na salama. 

Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza mabilioni ya fedha kuongeza huduma yam aji ili kuwafikia wananchi kwa huduma hii muhimu, ikiwemo miradi mingine kama ule wa Miji 28 ya Rorya, Tarime, Sirari hadi Mugumu.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb), amesisitiza: “Kumuenzi Mwalimu Nyerere ni kuwapelekea wananchi huduma ya majisafi, salama na ya kutosheleza, kwa sababu ndicho alichokisimamia katika maisha yake yote.”

Katika ziara ya ukaguzi hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amewataka watendaji kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma kwa wananchi. 

Kwa sasa takribani wananchi elfu tatu wameshaanza kunufaika moja kwa moja ambapo uzalishaji wa maji ukiwa lita milioni 17 kwa siku kiasi ambacho kinachoweza kuhudumia watu wengi zaidi. 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mugango–Kiabakari, Mhandisi Joel Rugemalila, anasema mradi huo utawanufaisha wananchi zaidi ya laki mbili wanaoishi Musoma Vijijini Butiama na baadhi ya maeneo ya Bunda mara utakapokamilika.

Shukrani kwa Serikali na viongozi zimekuwa zikisambaa miongoni mwa wananchi. Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwibara, John Waitare, anasema kuwa wananchi wameupokea mradi huo kwa mikono miwili. 

Naye mkazi wa Mugango, Mafuru Marambo, ameongeza kuwa mradi huo utamtua mama ndoo kichwani kama ahadi ya Serikali inavyosema.

Zaidi ya hudumaya maji kwa wananchi, mradi huo pia unaleta faraja na heshima. Wengine wanasema sasa watapata fursa ya kuoga nyumbani kwa faragha badala ya safari za ziwani, huku viongozi wa vijiji wakisisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu na vyanzo vya maji. 

“Mradi huu utakuwa na chujio na dawa za kutibu maji, hivyo ni jukumu letu wananchi kuwa walinzi wa mali hii,” Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kwibara, Hassan Maximillian anasema.

Hata hivyo, changamoto mpya pia zinakuja. Ziwa Victoria linakabiliwa na uchafuzi na mabadiliko ya tabianchi. 

Hii inahitaji mshikamano wa kila mmoja kuanzia Serikali, wadau na wananchi ili kulinda chanzo hiki kwa vizazi vijavyo. Hapa ndipo hekima ya Mwalimu inapotupa tena dira: rasilimali ni amana, si kwa kizazi kimoja, bali kwa vizazi vyote.

Katika Siku hii ya Nyerere, mradi wa maji wa Mugango–Kiabakari–Butiama unasimama kama kumbukumbu hai ya Baba wa Taifa. 

Wakati Watanzania wanapomkumbuka, wananchi wa Mara wanasherehekea kwa namna ya pekee: kwa kufungua bomba na kunywa majisafi na salama katika ardhi aliyozaliwa Mwalimu. Kitendo hicho cha kawaida kimejaa uzito wa historia na furaha ya maendeleo.

Hakika, maji yanayotiririka Butiama leo si maji tu, ni ndoto ya Serikali na Mwalimu Nyerere iliyotimia kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news