KERALA-Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya na mmoja wa waasisi wa demokrasia ya kisasa nchini, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga mwenye umri wa miaka 80 amefariki dunia leo Oktoba 15,2025 akiwa nchini India alipokuwa akipokea matibabu ya kiafya katika Jimbo la Kerala.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka hospitali ya Devamatha Medical College na vyombo mbalimbali vya habari, Mhe.Odinga alipata matatizo ya ghafla ya moyo alipokuwa akifanya mazoezi ya asubuhi ndani ya Hospitali ya Ayurvedic.
Hospitali ya Devamatha ndiyo ilithibitisha kifo chake baada ya kupelekwa huko kutoka Hospitali ya Ayurvedic.
Aidha,licha ya juhudi kubwa za madaktari na wauguzi, juhudi za kuokoa maisha yake hazikufanikiwa, na alitangazwa kufariki dunia majira ya saa tatu asubuhi kwa saa za India.
Mheshimiwa Raila Odinga alikuwa mtu wa maono, aliyejitolea kwa muda wa zaidi ya miaka 40 kutetea haki, demokrasia, usawa na maendeleo ya Kenya.
Kupitia chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM) na muungano wa Azimio la Umoja aliibuka kuwa kiongozi mashuhuri na mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Kenya.
Katika maisha yake ya kisiasa, Raila alihusishwa na harakati za mageuzi ya kikatiba, upatikanaji wa haki za kijamii, na kusimama kidete dhidi ya udikteta na ufisadi.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa taifa la Kenya, Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla. Amepumzika, lakini urithi wake utaendelea kuishi kupitia vizazi vilivyoongozwa na maono yake ya taifa lenye mshikamano, haki na maendeleo.
Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu wa Kenya kati ya 2008 na 2013, kipindi ambacho alisimamia juhudi za maridhiano ya kitaifa baada ya machafuko ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Ni kupitia makubaliano ya kugawana madaraka yaliyosimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kufuatia ghasia za uchaguzi wa mwaka 2007.
Aligombea Urais mara tano mwaka 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022, lakini hakuwahi kupata wadhifa huo licha ya kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya.
Raila Odinga ameacha mjane, Mama Ida Odinga, na watoto wanne akiwemo Raila Junior. Alikuwa mtu wa familia, mpenzi wa michezo, hususan soka, na mara kadhaa alionekana kuunga mkono timu za nyumbani katika mashindano mbalimbali.
