NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa wananchi wa Kenya kufuatia kifo cha kiongozi wa upinzani na mwanasiasa mashuhuri, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga leo Oktoba 15,2025 nchini India.
Kupitia taarifa rasmi aliyoitoa kupitia mitandao yake ya kijamii leo, Rais Dkt.Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Odinga.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemtaja Raila Amolo Odinga kuwa ni kiongozi mahiri, mpenda amani na mtafuta suluhu ambaye mchango uligusa ndani na nje ya mipaka ya Kenya.
“Tumempoteza kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,”amesema Dkt. Rais Samia.
Pia,Rais Dkt.Samia ameongeza kuwa,msiba huo si wa Kenya pekee bali wa bara la Afrika zima, kutokana na mchango mkubwa wa marehemu katika harakati za kidemokrasia, ushirikiano wa kikanda na amani barani.
Vilevile,katika salamu zake, Rais Dkt.Samia ametuma pole kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Dkt. William Samoei Ruto, mjane wa marehemu Mama Ida Odinga, familia ya Odinga na wananchi wote wa Kenya kwa ujumla.
“Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra, faraja na imani katika kipindi hiki, na ailaze roho ya mpendwa wetu Mheshimiwa Raila Amolo Odinga mahali pema peponi,” aliongeza.
Marehemu Raila Odinga alikuwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri na wenye ushawishi mkubwa katika historia ya kisiasa ya Kenya, aliyehudumu kwa zaidi ya miongo mitatu katika siasa za kitaifa, akishiriki mara kadhaa katika kinyang’anyiro cha urais na kushikilia nyadhifa mbalimbali za kitaifa.
Aidha,kifo chake kimejiri siku chache baada ya kaka yake, Dkt.Oburu Oginga kuthibitisha kuwa ndugu yake mdogo, Odinga alikuwa mgonjwa kwa muda, lakini alikuwa akiendelea kupata nafuu nchini India.
Kauli yake ilijiri siku chache baada ya uvumi na taarifa zinazokinzana kusambaa kuhusu hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa Chama Orange Democratic Movement (ODM).
Mbali na hayo,kupitia mahojiano na Radio Nam Lolwe, Dkt.Oginga alieleza kuwa,ugonjwa huo haukuwa wa kutishia maisha ya ndugu yake Raila Amolo Odinga.
“Raila, kama binadamu yeyote, alipata matatizo madogo ya kiafya siku chache zilizopita, lakini kwa sasa anaendelea vizuri. Alisafiri kwenda India kwa uchunguzi wa kiafya na sasa anapumzika,"alisema Dkt.Oginga ambaye pia ni msemaji wa familia ya Odinga.
Hata hivyo, kauli yake ilikinzana na ile ya mke wa Raila, Mama Ida Odinga ambaye hivi karibuni alikanusha madai kuwa mume wake ni mgonjwa, akieleza kuwa alichukua likizo fupi.
“Kama mtu ninayeishi naye kila siku, naifahamu afya yake vyema kuliko mtu mwingine yeyote. Haieleweki ni vipi mtu asiyeishi naye anaweza kudai anajua hali yake ya afya kuliko mimi. Ninachowaambia ndicho ukweli,”alisema Mama Ida Odinga.
Mheshimiwa Raila Odinga alikuwa mtu wa maono, aliyejitolea kwa muda wa zaidi ya miaka 40 kutetea haki, demokrasia, usawa na maendeleo ya Kenya.
Kupitia chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM) na muungano wa Azimio la Umoja aliibuka kuwa kiongozi mashuhuri na mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Kenya.
Katika maisha yake ya kisiasa, Raila alihusishwa na harakati za mageuzi ya kikatiba, upatikanaji wa haki za kijamii, na kusimama kidete dhidi ya udikteta na ufisadi.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa taifa la Kenya, Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla. Amepumzika, lakini urithi wake utaendelea kuishi kupitia vizazi vilivyoongozwa na maono yake ya taifa lenye mshikamano, haki na maendeleo.
Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu wa Kenya kati ya 2008 na 2013, kipindi ambacho alisimamia juhudi za maridhiano ya kitaifa baada ya machafuko ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Ni kupitia makubaliano ya kugawana madaraka yaliyosimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kufuatia ghasia za uchaguzi wa mwaka 2007.
Aligombea Urais mara tano mwaka 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022, lakini hakuwahi kupata wadhifa huo licha ya kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya.
Raila Odinga ameacha mjane, Mama Ida Odinga, na watoto wanne akiwemo Raila Junior. Alikuwa mtu wa familia, mpenzi wa michezo, hususan soka, na mara kadhaa alionekana kuunga mkono timu za nyumbani katika mashindano mbalimbali.
Wakati huo huo,Rais wa Kenya, Dkt.William Ruto ametangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku saba kufuatia kifo cha Raila Amolo Odinga ambapo bendera zote za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya heshima na maombolezo.
Dkt.Ruto ametangaza kusitisha shughuli zake zote za umma na kuwasihi maafisa wengine wa serikali kuchukua hatua kama hiyo ili kutoa nafasi ya kutafakari na kuomboleza maisha ya kiongozi huyo mashuhuri ndani na nje ya Kenya.
Tags
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Kimataifa
Raila Amolo Odinga
Raila Odinga Afariki
Waziri Mkuu wa Kenya
