MARA-Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewaongoza mamia ya wananchi na wachimbaji wadogo wa mgodi wa Ilasanilo katika maziko ya aliyekuwa Meneja wa mgodi huo, Isaya Daudi aliyefariki dunia Septemba 29 kwa ajali ya gari katika eneo la Bumangi wilayani Butiama.
Isaya Daudi alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ambapo katika maziko hayo, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa marehemu atakumbukwa kwa mchango mkubwa alioutoa katika kusaidia serikali kudhibiti upotevu wa maduhuri pamoja na kuimarisha usafi wa mazingira katika Mgodi wa Ilasanilo.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Amin Msuya, pia amethibitisha kuwa Isaya alisaidia sana mgodi huo na wachimbaji wadogo kushinda tuzo ya wachangiaji bora wa mrabaha wa serikali pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini.
Aidha, Katibu wa FFEMATA Mkoa wa Mara, Meshack Kabuta pamoja na Mwenyekiti wa Mgodi wa Ilasanilo, wameahidi kuendeleza miradi na juhudi zilizochukuliwa na marehemu Isaya katika enzi za uhai wake.Maziko haya yamebeba ujumbe wa mshikamano na kuenzi jitihada za watu waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya madini mkoani Mara.


