ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza sera ya utoaji wa asilimia 80 ya bei ya zao la karafuu kwa mkulima, hatua inayolenga kuinua kipato cha wakulima na kuchochea uzalishaji wa zao hilo muhimu la biashara.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 23,2025 katika hafla ya kukabidhi hati miliki za mashamba kwa wakulima wa karafuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Umoja ni Nguvu wa Baraza la Mji Mkoani, Pemba.
Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kutambua umuhimu wa zao la karafuu katika uchumi wa Zanzibar na maisha ya wananchi wake, na itaendeleza juhudi za kuongeza uzalishaji na thamani ya zao hilo ili liwe na tija zaidi kwa taifa na wakulima kwa ujumla.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amekabidhi boti ya wagonjwa (ambulance boat) kwa ajili ya wananchi wa visiwa vya Panza na Makoongwe, ikiwa ni juhudi za Serikali kuboresha huduma za afya na usafiri wa wagonjwa katika maeneo hayo ya visiwani.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Bandari ya Mkoani.Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amekabidhi gari kwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kwa lengo la kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa mashamba ya karafuu katika maeneo mbalimbali ya Pemba na Unguja.


















