Taarifa muhimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu upotoshaji fedha zinazochapishwa na BoT pamoja na ushawishi wa kuondoa fedha kwenye mabenki

NA DIRAMAKINI

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amekanusha vikali taarifa zinazosambaa mitandaoni zinazoeleza kuwa, benki hiyo imechapisha na kusambaza fedha kwa ajili ya kugharamia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Kupitia taarifa kwa umma aliyoitoa leo Oktoba 17,2025, Gavana Tutuba ameeleza kuwa, taarifa hizo ni za upotoshaji na hazina ukweli wowote.

Amesisitiza kuwa, Benki Kuu hufanya uchapishaji wa fedha kwa mujibu wa sheria, hasa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, Sura ya 197, na hufanya hivyo kwa kuzingatia hali ya uchumi na mahitaji halali ya mzunguko wa fedha.

“Napenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa taarifa hizo siyo za kweli, zinapaswa kupuuzwa na tunawataka wanaozisambaza waache mara moja,”amesisitiza Gavana Tutuba.

Aidha, amebainisha kuwa hali ya uchumi wa nchi kwa sasa ni imara, huku viashiria vikuu vya kiuchumi vikionesha mafanikio makubwa.

Pia,mfumuko wa bei umetajwa kuwa wa chini kwa wastani wa asilimia 3.3 kwa miezi 10 ya mwaka 2025, ukuaji wa uchumi unatarajiwa kufikia asilimia 6, huku akiba ya fedha za kigeni ikifikia Dola za Marekani bilioni 6.7, inayokidhi uagizaji wa bidhaa kwa miezi 5.4.

Gavana pia amepuuza madai kuwa baadhi ya benki za biashara zimeishiwa fedha, akisisitiza kuwa taasisi zote za kifedha nchini zipo imara, zina ukwasi na mitaji ya kutosha, na zinaendelea kutengeneza faida.

Ameongeza kuwa, kiwango cha mikopo chechefu kimeendelea kuwa chini, kufikia asilimia 3.3 mwezi Septemba 2025, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 5.0.

Katika hatua nyingine,Gavana Tutuba ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuamini mfumo wa kibenki na kuacha tabia ya kuondoa fedha kutoka benki kwa sababu za hofu zisizo na msingi.

“Uamuzi wa kutunza fedha nyumbani ni wa kizamani na una hatari nyingi zikiwemo kuibiwa, kupotea au kuungua moto.”

Benki Kuu imewahakikishia wananchi kuwa mifumo yote ya malipo inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na usalama, huku ikiwataka Watanzania waendelee kutumia huduma za benki kwa utulivu.

Vilevile,Gavana Tutuba ametoa onyo kali kwa watu wote wanaoeneza taarifa za upotoshaji mitandaoni, akiwataka kuacha mara moja kwani vitendo hivyo vinaathiri sekta ya fedha na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news