Tanzania ya kwanza nchi za Maziwa Makuu kutoa vyeti na kufanya ukaguzi wa meli

DAR-Wataalam 45 wa Afya Mipaka ya Bandari Nchini wako jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mafunzo yanayotolewa na wataalamu wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kuwajengea uwezo wa kufanya ukaguzi wa Meli kwa kutumia kanuni za shirika hilo kudhibiti magonjwa ya mlipuko kutoka Nchi nyingine.
Dkt. Amour Selemani Mkuu wa Huduma za Afya Mipakani kutoka Wizara ya Afya akiongea na mwandishi wa habari hii kuhusu mafunzo haya leo Oktoba 21, 2025 jijini Dar es Salaam amesema mafunzo haya yanaipa Tanzania uwezo wa kutambulika Kimataifa kutoa vyeti vya Usafi na Mzingira.

Aidha Dkt. Amour ameongeza kuwa, kutokana na ongezeko la watu na Maendeleo ya Kiteknolojia kunapelekea mwingiliano watu kutoka eneo moja kwenda lingine na hivyo kuongezeka kwa hatari ya magonjwa ya mlipuko katika maeneo ya mipakani.
Kanuni zitakazotumiwa na wataalam hawa ni kanuni za mwaka 2005 (IHR 2005) zilizoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuridhiwa na Nchi Wanachama wa shirika hilo zitakazo tumiwa na wataalam wa ndani kutoa cheti cha usafi na mazingira baada ya kukamilisha zoezi la ukaguzi kwa meli husika.

‘’Wizara ya Afya imeandaa mafunzo haya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa hitaji la wataalam wenye uwezo wa kutambua na kudhibiti magonjwa ya mlipuko kama ilivyoagizwa na Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko wakati akifungua Mradi wa Uhimarishaji Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko Maarufu Pandemic Fund hivi karibuni jijini Mwanza’’, anasema Dkt. Amour.
Kuhusu vitendea kazi Dkt. Amour amesema tayari vifaa vinavyotumika kutambua na kudhibiti magonjwa kwa kuanzia vipo tayari lakini vifaa zaidi vipo katika machakato wa kununuliwa kwa ufadhili WHO kupitia mradi wa Uhimarishaji Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko unaotekelezwa na shirika hilo.

Naye Dkt. George Kauki Afisa Ufuatiliaji wa magonjwa ya Mlipuko kutoka WHO-Tanzania amesema mafunzo kwa wataalam hawa kimsingi yametumia hatua kadhaa ya kimaandalizi ikiwemo yale ya njia ya mtandao, yakifuatiwa na hatua ya pili ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya yaliyolenga kuwajengea uwezo kulingana na mazingira yetu ya ndani.

Dkt. Kauki pia amebainisha kuwa ili wataalam hawa wa Afya waweze kufanya ukaguzi na kutoa cheti inabidi wapate mafunzo kutoka kwa wataalam waliodhinishwa na WHO akiyataja kuwa hatua muhimu inayoifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa ukanda wa maziwa makuu kuwa na wataalam wenye uwezo kufanya ukaguzi na kutoa vyeti kwa meli zitakazo kuwa zinatumia bandari hapa Nchini.
Wataalam wa mafunzo haya muhimu wanatoka Tanzania bara na Zanzibar kwa bandari za Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Tanga na kwa upande wa Zanzibar washiriki wanatoka bandari za Malindi, Wete, Mkoani,Fumba na Mkokotoni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news