Tuipende nchi yetu

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Oktoba 14,2025 ni kumbukizi ya miaka 26 tangu alipofariki Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Siku hii huadhimishwa kila mwaka Oktoba 14, ikiwa ni siku aliyofariki dunia mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London,Uingereza.

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika Kijiji cha Butiama Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Tanzania (wakati ule ilikuwa Tanganyika).

Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa na kuenziwa na vizazi baada ya vizazi kwa kuwa kiongozi mahiri, mpatanishi, kiunganishi na mzalendo aliyelipenda na kulitumikia Taifa lake kwa namna zote.

Pia, alikuwa na uwezo wa kuona mbali, hata alipopingwa baadaye waliompinga walikiri ukweli wa maono yake, kwani alisimamia maadili na uongozi wa haki, umoja wa Kitaifa, kujitegemea, kupinga rushwa na mengineyo.

Katika moja ya hotuba zake Julai 29,1985 alinukuliwa akisema kuwa,"kazi iliyokuwa muhimu kuliko zote kwangu mimi, ilikuwa ni kujenga Taifa lenye umoja kwa msingi wa heshima na usawa wa binadamu."

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ili kuendelea kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kila mmoja wetu ana wajibu wa kuipenda nchi yetu ya Tanzania.

Anasema, Mwalimu Nyerere aliipenda Tanzania kwa dhati na mapenzi hayo yalidhihirika si kwa maneno tu, bali kwa matendo yake katika maisha yote ya uongozi.Endelea;

1.Vile wampenda mama, vivyo hivyo penda nchi,
Si mimi ninayesema, alisema mwenye nchi,
Yeye alishika tama, huku aiaga nchi,
Huu wosia wa baba, Mwalimu J. Nyerere.

2.Huu wosia wa baba, Mwalimu J. Nyerere,
Siku zipokuwa haba, kifo kikiwa ni sare,
Alituusia baba, hiyo hekima ya bure,
Vipi waipenda nchi, ndivyo wampenda mama?

3.Vipi waipenda nchi, ndivyo wampenda mama?
Wewe ndiye mwananchi, nchi aliacha njema,
Umekaa kwenye kochi, nchi bora kama mama?
Aliyosema Nyerere, hebu rudia rudia.

4.Aliyosema Nyerere, hebu rudia rudia,
Wala usiseme sore, nchi ukiibia,
Ni bora uone gere, kunyonya ukiachia,
Mama aweza toweka, nchi iko pale pale.

5.Mama aweza toweka, nchi iko pale pale,
Yuko hai furahika, nchi bado iko pale,
Amekufa sikitika, nchi iko pale pale,
Nchi unapoipenda, pendo lizidi la mama.

6.Nchi unayoipenda, pendo lizidi la mama,
Kinamama wanakwenda, wanatuachia homa,
Na kinababa waenda, tunabakia yatima,
Nyerere lishaondoka, bado ipo Tanzania.

7. Nyerere lishaondoka, bado ipo Tanzania,
Hii haitatoweka, hadi mwisho wa dunia,
Sisi tutabadilika, wengine watasalia,
Tuipende nchi yangu, kama kupenda wazazi.

8.Tuipende nchi yetu, kama kupenda wazazi,
Hapo tutakuwa watu, kama tunachapa kazi,
Yoyote yaliyo butu, tusifanye kwetu dozi,
Tanzania Tanzania, tuipende nchi yetu.

9.Tanzania Tanzania, tuipende nchi yetu,
Tufanye mambo kwa nia, tusiharibu misitu,
Kodi kutoilipia, tusiendekeze katu,
Alituasa Mwalimu, watuasa viongozi.

10.Alituasa Mwalimu, watuasa viongozi,
Hayo maonyo adhimu, vema kufanyia kazi,
Tanzania itadumu, uchumi kipanda ngazi,
Ya kale kweli dhahabu, twajifunza kwa Nyerere.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news