Tume yatangaza marekebisho ya maeneo ya uchaguzi,yatengua wagombea

DAR-Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza mabadiliko kwenye orodha ya maeneo ya uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa kata 10, wagombea saba wa udiwani na vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwapo katika kata hizo.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 12, 2025 wakati akitangaza orodha ya maeneo ya uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kufuatia kufutwa kwa baadhi ya maeneo na kutangaza kutengua uteuzi wa wagombea saba katika maeneo ya uchaguzi yaliyofutwa, kufutwa kwa vituo vya kupigia kura 292 na kuanzishwa kwa vituo vingine 292 katika kkata walipohamishiwa wapiga Kura husika. (Picha na INEC).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema, mabadiliko hayo ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kupitia Matangazo ya Serikali Na. 596 na Na. 600 ya Oktoba 3, 2025, yaliyotangaza baadhi ya maeneo kuwa tengefu kwa makazi ya wakimbizi na kufuta kata kadhaa katika mikoa ya Katavi na Tabora.

“Tume, katika kikao chake cha Oktoba 6, 2025 na kwa kuzingatia Tangazo la Serikali Na. 604 la Oktoba 10, 2025, imefanya maamuzi yafuatayo: Kwanza, kuzifuta rasmi kata kumi zilizofutwa na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa katika orodha ya maeneo ya uchaguzi wa madiwani kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025. Pili, kutengua uteuzi na kuwaondoa wagombea saba wa udiwani waliokuwa wamepita katika kata husika,” amesema Jaji Mwambegele.

Kata zilizofutwa ambazo baadhi zilikuwa na wagombea walioteuliwa ni Litapunga, Kanoge, Katumba, Mishamo, Ilangu, Bulamata na Ipwaga. Kata nyingine zilizofutwa lakini hazikuwa na wagombea ni Milambo, Igombemkulu na Kanindo.

Kutokana na hatua hiyo, vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa kwenye kata hizo vimeondolewa rasmi, na vituo vingine 292 vimeanzishwa katika kata za jirani ili kuhakikisha wapiga kura wanaendelea kutumia haki yao ya kikatiba.

“Wapiga kura 106,288 waliokuwa wakihudumiwa na vituo vilivyofutwa wamehamishiwa kwenye vituo vipya vilivyoanzishwa katika kata za Mtapenda, Uruwira, Nsimbo na Ugala zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mkoa wa Katavi. Vilevile, baadhi wamehamishiwa katika kata za Sasu, Ilege, Uyowa, Makingi na Silambo zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora, pamoja na Kata ya Tongwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Mkoa wa Katavi,” amesema.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news