DODOMA-Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ratiba mpya ya uchaguzi katika maeneo yaliyositishwa kutokana na vifo vya baadhi ya wagombea. Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo, kupiga kura katika maeneo husika kutaendeshwa tarehe 30 Desemba,2025.
Uchaguzi huo utahusisha Jimbo la Fuoni, Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar, kufuatia kifo cha Kapteni Abbas Ali Mwinyi, aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichotokea Septemba 25, 2025.
Kata ya Chamwino, Jimbo la Morogoro Mjini na Kata ya Mbagala Kuu, Jimbo la Mbagala, ambako pia wagombea wa nafasi ya udiwani walifariki dunia, hivyo kusababisha kuahirishwa kwa uchaguzi katika maeneo hayo.
Tume imesisitiza kuwa uamuzi huu umezingatia masharti ya Kifungu cha 68(1), (3), (4) na 71(2) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.
INEC imewataka wadau wote wa uchaguzi kuzingatia ratiba hiyo mpya na kufuata taratibu za uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

Tags
Habari
INEC Tanzania
Jimbo la Fuoni
Kata ya Chamwino
Kata ya Mbagala Kuu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi

