NA GODFREY NNKO
KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania imekutana Oktoba 1,2025 na kuamua kuendelea kudumisha kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa asilimia 5.75 katika Robo ya Nne ya 2025.
Uamuzi huu umetokana na tathmini ya kina kuhusu mwenendo wa mfumuko wa bei na hali ya uchumi kwa ujumla, ambapo viashiria vinaonesha kuwa mfumuko wa bei utabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, na uchumi wa taifa utaendelea kuwa thabiti.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 02,2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Emmanuel Tutuba ambaye pia ni Gavana wa BoT wakati akizungumza katika mkutano na viongozi wa benki, taasisi za fedha na waandishi wa habari.
Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) ni kiwango kinachowekwa na BoT kama rejea katika utekelezaji wa shughuli zake mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukopesha benki za biashara.
Aidha, kiwango hiki huathiri riba za mikopo baina ya benki za biashara, ambazo zinapaswa kuwa ndani ya wigo wa asilimia ±2.0 ya CBR iliyowekwa.
Gavana Tutuba amesema, tathmini ya taasisi za kimataifa za Moody’s na Fitch Ratings imetoa picha chanya ya uchumi wa Tanzania, kwa kuipatia daraja la B1 na B+, mtawalia. Hili linathibitisha kuwa msingi wa uchumi wa nchi umeendelea kuimarika.
Amesema, Benki Kuu itaendelea kutekeleza sera ya fedha kwa kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya mabenki (7-day interbank rate) inabaki ndani ya wigo wa asilimia ±2 ya CBR.
Katika robo mwaka iliyoishia Septemba 2025, Gavana Tutuba amesema, utekelezaji wa sera hii ulifanikiwa kwa kiwango kikubwa, na kuimarisha ukwasi katika mfumo wa kifedha, huku riba za mikopo zikipungua na kukaribia kiwango cha CBR kwa kipindi kikubwa cha robo hiyo.
Licha ya kupungua kwa kasi ya ukuaji katika nchi zilizoendelea na zinazoibukia katika robo ya tatu ya 2025, hali ya uchumi wa Dunia inaonesha matumaini ya kuimarika katika robo ya mwisho ya mwaka.
Amesema,benki kuu nyingi duniani zimeamua kuacha au kupunguza viwango vya riba ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Pia, amefafanua kuwa,bei ya bidhaa duniani, hususan mafuta ghafi, zilipungua hadi wastani wa dola 68 kwa pipa, hali iliyoleta nafuu kwa mataifa yanayoagiza bidhaa hiyo, ikiwa ni pamoja na Tanzania.
Bei ya dhahabu iliendelea kuwa juu, ikifikia wastani wa dola 3,354.1 kwa wakia, na inatarajiwa kubaki katika viwango hivyo au kuongezeka kidogo.
Tanzania Bara ilishuhudia mfumuko wa bei wa asilimia 3.4 mwezi Agosti 2025, kiwango kinachobakia ndani ya lengo la kitaifa na kikanda EAC na SADC.
Gavana Tutuba amesema, hili lilichangiwa na sera madhubuti za fedha na bajeti, upatikanaji wa chakula wa kutosha, utulivu wa thamani ya shilingi na kupungua kwa bei ya mafuta.
Aidha,Shilingi ya Tanzania iliendelea kuwa imara, ikiongezeka thamani kwa asilimia 8.4 katika robo ya tatu ya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 0.7 katika robo iliyotangulia.
Kwa upande wa akiba ya fedha za kigeni, Gavana Tutuba amesema, ilifikia dola bilioni 6.7 mwishoni mwa Septemba 2025, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi mitano.
Vilevile, amesema katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.2 mwaka uliotangulia.
Mwenendo huu ulichangiwa zaidi na shughuli za uchimbaji madini, kilimo, huduma za fedha na bima, ujenzi, na shughuli za uzalishaji viwandani.
Benki Kuu ya Tanzania inakadiria uchumi kuendelea kuimarika, ukikua kwa zaidi ya asilimia 6 katika robo ya pili na ya tatu ya mwaka 2025.
Ukuaji katika robo ya nne ya mwaka 2025 unatarajiwa pia kuwa na mwenendo wa kuridhisha.
Matarajio haya yanachagizwa na uwekezaji unaofanywa na Serikali pamoja na sekta binafsi, na ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.
Katika robo mwaka iliyoishia Septemba 2025, ujazi wa fedha ulikua kwa wastani wa asilimia 20.4, ikilinganishwa na asilimia 19.1 katika robo iliyotangulia.
Gavana Tutuba amesema,mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 16, huku mikopo chechefu ikishuka hadi asilimia 3.3 ikiwa ni chini ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 5.
Aidha,sekta ya nje ya uchumi wa Tanzania ilipata nguvu kutokana na ongezeko la mauzo ya mazao ya biashara, dhahabu na utalii.
Nakisi ya urari wa malipo ya kawaida ilipungua hadi asilimia 2.4 ya Pato la Taifa kwa mwaka ulioishia Septemba 2025, kutoka asilimia 3.8 mwaka uliotangulia.
Kuhusu utekelezaji wa bajeti kwa Tanzania Bara na Zanzibar, Gavana Tutuba amesema, ulikuwa wa kuridhisha.
Amesema, mapato ya ndani yalivuka malengo kutokana na makusanyo bora ya kodi, yaliyochangiwa na utayari wa walipakodi na usimamizi bora.
Pia,matumizi ya serikali yaliendana na rasilimali zilizopo huku deni la taifa lilibaki kuwa katika viwango vya kudhibitika,na sehemu kubwa ya fedha za mikopo zimewekezwa kwenye miradi ya kimkakati ya miundombinu.
Gavana Tutuba amesema,Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia kukutana tena Januari 7, 2026, ambapo uamuzi mpya kuhusu Riba ya Benki Kuu ya CBR utatangazwa Januari 8, 2026.


