WIZARA ya Fedha ilianzishwa mara tu baada ya Uhuru mnamo mwaka 1961. Imepitia mabadiliko kadhaa yaliyolenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli za Serikali.
Mabadiliko hayo yalilenga kipengele cha uongozi, majukumu na jina la Wizara. Mnamo mwaka 1962 iliitwa Wizara ya Fedha; Mwaka 1967 Wizara ya Fedha na Mipango; Mwaka 1983 Wizara ya Nchi, Mipango na Uchumi; 2008 Wizara ya Fedha na Uchumi; Mwaka 2010 Wizara ya Fedha; Mwaka 2015 Wizara ya Fedha na Mipango na Mwezi Julai Mwaka 2023 ikabadilishwa kuwa Wizara ya Fedha.
Wizara ya Fedha inasimamia Mapato, Matumizi na fedha zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inaipa Serikali ushauri kuhusu masuala mapana ya Fedha na Uchumi katika kuunga mkono malengo ya Serikali ya kukuza uchumi na jamii.
Wizara ya Fedha pia ni chombo chenye mamlaka ya kusimamia: uundaji wa sera za kodi na udhibiti wa fedha, mapato, benki, bima, uhasibu, manunuzi ya umma, mikopo na sera za mikopo, kufuatilia utekelezaji wake, uratibu wa fedha na misaada kutoka nje ya nchi, ushuru, na masuala ya kubadilisha fedha za kigeni, ambapo ili kufanikisha kazi zote, Wizara imegawanyika katika idara na vitengo mbalimbali kama ifuatavyo:
- Idara ya Uchambuzi wa Sera,
- Idara ya Usimamizi wa Madeni
- Idara ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha
- Idara ya Fedha za Nje,
- Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali,
- Idara ya Sera ya Manunuzi ya Umma,
- Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali
- Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali,
- Idara ya Mifumo ya Usimamizi wa Fedha na Huduma za Tehama,
- Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali,
- Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu,
- Idara ya Mipango,
- Idara ya Huduma za Kisheria,
- Kitengo cha Fedha na Uhasibu
- Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani
- Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi,
- Kitengo cha Usimamizi na Ununuzi
- Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
- Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini

















