ZANZIBAR-Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa sasa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea kutekeleza na kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo kwa lengo la kuwaletea ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Akihutubia maelfu ya wakazi wa Paje leo Oktoba 16,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Paje, Dkt.Mwinyi amesema,miradi hiyo inalenga sekta muhimu kama vile miundombinu, elimu, afya na maji ambazo ni msingi wa maendeleo ya watu.
Akihutubia maelfu ya wakazi wa Paje leo Oktoba 16,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Paje, Dkt.Mwinyi amesema,miradi hiyo inalenga sekta muhimu kama vile miundombinu, elimu, afya na maji ambazo ni msingi wa maendeleo ya watu.“Tumejipanga kukamilisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Tunguu hadi Makunduchi, sambamba na barabara za ndani za Mkoa wa Kusini Unguja,”amesema Dkt.Mwinyi.
Aidha, ametaja ujenzi wa madaraja muhimu yatakayounganisha mikoa ya Kusini na Kaskazini, ikiwemo daraja la Unguja Ukuu–Uzi–Ng’ambwa na la Chwaka–Charawe, kuwa ni kipaumbele katika awamu ijayo ya uongozi wake.Katika sekta ya usafiri wa majini na anga, Serikali imepanga kukamilisha Bandari ya Kizimkazi pamoja na kuimarisha bandari ndogo za Mtene, Chwaka na Unguja Ukuu.
Pia, ujenzi wa viwanja vya ndege vya Nungwi na Paje umetajwa kuwa chachu ya kukuza ajira na biashara visiwani.
Akizungumzia sekta ya elimu, Dkt.Mwinyi amesema, "Tutaendelea kujenga madarasa 1,000 kwa shule za msingi na 1,000 kwa sekondari, pamoja na shule za kisasa za ghorofa ili kuongeza fursa za elimu bora kwa watoto wetu.”
Kwa upande wa afya, Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,Serikali itajenga Hospitali ya Mkoa wa Kusini Unguja, huku Hospitali ya Rufaa ya Kufundishia Binguni na Hospitali ya Saratani zikiendelea kwa kasi nzuri ya utekelezaji.Katika kuhakikisha huduma za maji safi na salama zinawafikia wananchi wa Kusini Unguja, Dkt.Mwinyi alieleza kuwa,mradi wa dola milioni 55 za Marekani utawezesha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa maeneo ya Uroa, Marumbi, Pongwe, Jambiani na Makunduchi.
Kwa upande wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, aliahidi kuendelea kutoa mafunzo, mikopo isiyo na riba, na vifaa vya uzalishaji kwa wananchi ili wachangamkie fursa za kiuchumi zitokanazo na miradi hiyo.
Dkt. Mwinyi ameendelea kuwasihi wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano, huku akiwaomba kumpa tena ridhaa ya kuiongoza Zanzibar kwa muhula mwingine ili akamilishe miradi iliyoanzishwa.
“Naomba muendelee kuniamini na kunipa ridhaa ya kuiongoza Zanzibar kwa muhula mwingine ili tukamilishe miradi hii mikubwa na kuleta ustawi zaidi kwa wananchi wetu wote,”amesema Dkt.Mwinyi.
















