Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yafikisha tani 15.37 za dhahabu

MWANZA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa hadi sasa Benki Kuu imenunua jumla ya tani 15.37 za dhahabu kupitia mpango wake wa ununuzi wa madini hayo, ikiwa ni hatua muhimu ya kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya shilingi.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu katika mikoa ya Mwanza na Geita tarehe 26 Novemba 2025, ziara iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambaye pia ni Gavana.

Katika hatua ya kwanza ya ziara hiyo, Bodi ilitembelea ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ambaye alieleza kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati unaendelea vizuri, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na ujenzi wa jengo la abiria na mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutaimarisha mchango wa Mkoa wa Mwanza katika pato la taifa.

Aidha, Mhe. Mtanda alibainisha kuwa kukamilika kwa Daraja la J.P. Magufuli pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya meli kubwa katika Ziwa Victoria kumechochea ukuaji wa biashara kati ya Mkoa wa Mwanza na nchi jirani ya Uganda.

Katika Mkoa wa Geita, Bodi ilipokelewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa, Mhe. Hashim Komba, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita. Mhe. Komba aliipongeza Benki Kuu kwa utekelezaji mzuri wa mpango wa ununuzi wa dhahabu pamoja na ushiriki wake katika Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kila mwaka mkoani humo.
Alisema hatua hizo zimeongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta ya madini na kuchochea maendeleo ya wachimbaji wadogo na wa kati.


Ziara iliendelea hadi Geita, ambako Bodi ilitembelea Soko la Madini la Geita na Kiwanda cha Geita Gold Refinery, na kupata maelezo kuhusu mwenendo wa biashara ya madini na maendeleo ya teknolojia za uchakataji dhahabu katika maeneo hayo.
Ziara hii imetoa nafasi muhimu ya kufuatilia mwenendo wa miradi ya kimkakati pamoja na kujionea moja kwa moja mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news