MWANZA-Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, imefanya ziara katika mikoa ya Mwanza na Geita tarehe 26 Novemba 2025 kwa ajili ya kukagua na kujionea utekelezaji wa miradi ya kiuchumi katika maeneo hayo.
Katika ziara hiyo, Bodi ilipokelewa mkoani Mwanza na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Said Mtanda, ambaye alieleza kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati unaendelea kwa kasi.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), pamoja na ujenzi wa jengo la abiria na mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutaimarisha mchango wa mkoa huo katika pato la taifa.
Aidha, Mhe. Mtanda alibainisha kuwa kukamilika kwa Daraja la J.P. Magufuli pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya meli kubwa katika Ziwa Victoria kumechochea ukuaji wa biashara kati ya Mkoa wa Mwanza na nchi jirani ya Uganda.
Katika Mkoa wa Geita, Bodi ilipokelewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa, Mhe. Hashim Komba, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita.
Mheshimiwa Komba aliipongeza Benki Kuu kwa utekelezaji mzuri wa mpango wa ununuzi wa dhahabu pamoja na ushiriki wake katika Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kila mwaka mkoani humo.
Alisema hatua hizo zimeongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta ya madini na kuchochea maendeleo ya wachimbaji wadogo na wa kati.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Gavana Tutuba alisema,Benki Kuu inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, ikiwa ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei ili kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa taifa. 

Kuhusu mpango wa ununuzi wa dhahabu, Gavana Tutuba alibainisha kuwa hadi sasa Benki Kuu imenunua tani 15.37 za dhahabu kwa lengo la kuongeza akiba ya fedha za kigeni kupitia dhahabu na kuimarisha thamani ya shilingi.
Vilevile, katika ziara hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya BoT ilitembelea Soko la Madini la Mwanza pamoja na Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery.
Aidha, Bodi ilifika pia katika Soko la Madini la Geita na kutembelea Kiwanda cha Geita Gold Refinery, ambapo ilipata maelezo kuhusu mwenendo wa biashara ya madini na maendeleo ya teknolojia za uchakataji dhahabu katika maeneo hayo.








